RC Makonda awataka wakazi wa Dar kuwa na bima ya afya

Tuesday August 27 2019
makonda pic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wakazi wa mkoa huo kutambua kuwa bima ya afya ni moja ya vitu muhimu wanavyopaswa kuwa navyo.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 27, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili  (MNH) alipokutana na Ashraf Patrick, aliyemsaidia kufanyiwa upasuaji wa uvimbe usoni katika hospitali hiyo.

Patrick, mkazi wa Bukoba mkoani Kagera video zake zilisambaa katika mitandao ya kijamii akiomba msaada wa matibabu ya uvimbe huo, Makonda alimleta MNH na kufanyiwa upasuaji.

Makonda amesema Patrick angekuwa na bima ya afya asingelazimika kuomba msaada wa matibabu.

”Kuomba msaada au kulalamikia gharama za matibabu hakuwezi kuwepo kama una bima ya afya, huu ni msaada mkubwa sana,” amesema Makonda.

Amesema Dar es Salaam umewekwa utaratibu mzuri na nafuu wa bima ya afya na kuwataka ambao hawana kuhakikisha wanakuwa na bima ili kupata uhakika wa matibabu.

Advertisement

Naye daktari bingwa wa masikio, pua na koo,  Edwin Liyombo amesema upasuaji aliofanyiwa Patrick ulikuwa mkubwa.

“Tulimchunguza tukagundua kuwa ni saratani, tukaona tumfanyie upasuaji na kuondoa uvimbe. Kinachofanyika sasa ni kuendelea na matibabu na atahamishiwa kwenye taasisi ya saratani ya Ocean Road,” amesema Liyombo.

 

Advertisement