VIDEO: RC Mbeya aruhusu wanafunzi nane wafukuzwe shule

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila akiwa na kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa huo wakikagua maendeleo ya ukarabati wa mabweni mawili ya Shule ya Sekondari Kiwanja Wilayani Chunya,  leo. Mabweni hayo yaliteketea kwa moto baada ya wanafunzi wa shule hiyo wa kidato cha tano na sita kuchoma usiku wa kuamkia Septemba 30 mwaka huu, Picha na Godfrey Kahango.

Chunya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amebariki  wanafunzi wanane wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya kufukuzwa shule kwa tuhuma za kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo.

Kati ya wanafunzi hao, saba wanakabiliwa na kesi  mahakamani ya kuchoma mabweni hayo huku mmoja akitoroka baada ya kukutwa na simu na kondomu siku aliporipoti shuleni.

Chalamila ameeleza hayo leo Jumatano Oktoba 23, 2019  baada ya kufika katika shule hiyo kukagua ukarabati wa mabweni yaliyochomwa moto usiku wa kuamkia Septemba 30, 2019.

Amesema baada ya uchomaji moto huo wanafunzi saba walifunguliwa kesi mahakamani, kwamba bodi ya shule kabla ya kuvunjwa ilitoa uamuzi wa kuwafukuza shule wanafunzi hao.

Amesema mwanafunzi mmoja kati ya waliorudishwa nyumbani na kutakiwa kuripoti shuleni Oktoba 18, 2019 wakiwa wamelipa Sh200,000 kila mmoja, alikutwa na kondomu katika begi lake pamoja na simu.

Amesema mwanafunzi huyo baada ya kukutwa na vitu hivyo alikimbia na hadi leo hajarejea hivyo naye amefukuzwa rasmi.

Amesema baadhi ya wanafunzi wamelipa kiasi hicho cha fedha na wengine wamelipa nusu, kuwaongezea wiki moja kumaliza kiasi hicho cha fedha akisisitiza kuwa watakaoshindwa hawatatakiwa kuonekana katika shule hiyo.

“Nawaruhusu kuendelea na masomo hadi Novemba Mosi na watakapokuja hapa wawe na mambo mawili, kwanza ni barua ya kwa nini wamechelewa kuripoti shuleni na sababu za kufanya vurugu na pili wakiwa na fedha hizo.”

“Wanafunzi 14 ambao niliwacharaza bakora hapa (shuleni) niliwaambia wabaki kwa sababu ya kutoa ushahidi na waliutoa vizuri,” amesema Chalamila.

Ameongeza, “wazazi wao wameomba wiki moja kuanzia sasa  watakuwa wamewalipia  Sh500.000 kila mmoja. Hadi sasa wamelipa watano tu, na wao wataendelea na masomo kwa sababu tuliwaweka hapa kwa ajili ya kutoa ushahidi.”

Mkuu wa Shule hiyo, Elly Mnyarape amemueleza Chalamila kwamba  kati ya wanafunzi 390 waliorudishwa nyumbani, 362 wamesharejea shuleni hapo kuendelea na masomo huku Sh76. 2 milioni zikikusanywa.