RC Mbeya awapa mpaka saa 10 leo wanafunzi 59 kufutwa shule

Monday October 21 2019

 

By Godfrey Kahango, Mwananchi [email protected]

Rungwe. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ametishia kuwafukuza wanafunzi 59 wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja ya wilayani Chunya, ambao bado hawajalipa fedha.

Wanafunzi hao mpaka Ijumaa walikuwa hawajalipa fedha kama fidia ya mabweni mawili yaliyoungua.

Chalamila alisema wasipolipa mpaka leo saa 10 jioni atawafukuza kabisa shule, atawakamata, kuwafunga na kutowaruhusu kufanya mitihani yao ya mwisho kwa muda wa miaka mitano.

Alitoa kauli hiyo juzi jioni kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kibatata, kata ya Kisondola na alipozungumza na wanafunzi na wazazi wa Shule ya Sekondari Lutengano kwenye mahafali ya kidato cha nne.

Wanafunzi 300 wa kidato cha tano na sita wa Sekondari Kiwanja walifukuzwa shuleni hapo na Chalamila Oktoba 3 baada ya kutuhumiwa kuchoma mabweni mawili ya shule hiyo huku baadhi yao wakikamatwa na walimu wakimiliki simu kinyume na sheria na taratibu za shule hiyo.

Katika sakata hilo, Chalamila aliwacharaza bakora wanafunzi 14 waliokutwa wanamiliki simu, huku wanafunzi watano wakifikishwa mahakamani wakikabiliwa na kosa la kuchoma moto mabweni hayo.

Advertisement

Mkuu huyo wa mkoa baadaye aliwatimua shuleni wanafunzi wote 300 wa kidato cha tano na sita na kuwataka warejee shuleni Oktoba 18, huku wakiwa wamelipa kila mmoja Sh200,000 na wanafunzi watano walitakiwa kulipa Sh500,000 kila mmoja.

Akizungumza juzi, Chalamila alisema kati ya wanafunzi hao, wanafunzi 59 bado hawajarejea shuleni na hawajalipa fedha hivyo aliwatangazia kuwapa siku mbili kuanzia juzi kwamba ifikapo leo saa 10 jioni wawe wamelipa fedha na kurejea shuleni, vinginevyo atawafukuza kabisa shuleni, kuwafunga mahakamani na atawazuia kutofanya mitihani yao kwa muda wa miaka mitano.

“Hadi jana (Ijumaa) wamelipa wanafunzi 270, kila mmoja Sh200,000 na wale wengine Sh500,000 kila mmoja, lakini kuna vijana wengine kama 56, 59 hivi bado hawajalipa, ninawavizia hadi Jumatatu (leo) saa 10 jioni,” alisema.

“Ili kama hawajalipa, moja nitawafukuza shule, nitawakamata, nitawafunga na tatu hawataruhusiwa kufanya mitihani kwa muda wa miaka mitano toka sasa ili waonje joto la jiwe watakapokuwa mtaani ili wazazi pia wawe wanawaonya watoto wanapokuwa majumbani kwao,’’ alisema.

Akizungumzia ukarabati wa majengo yaliyochomwa moto, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, MaryPrisca Mahundi alisema wanafunzi 270 ndio walioripoti shuleni hapo wakiwa wamelipa fedha zote Sh200,000 kila mmoja lakini wanafunzi wengine 48 waliripoti shuleni hapo wakiwa na fedha pungufu na wengine wakiwa hawana kabisa fedha hivyo wakarudishwa majumbani kwao.

Alisema “hadi kufikia jana (juzi) asubuhi idadi ni hiyo waliokuwa wameripoti shule na wamelipa fedha lakini wengine pia waliendelea kuripoti shuleni hapo hadi jioni ya leo (jana) nitakuwa, nimepata idadi kamili.”

Alisema ukarabati wa mabweni hayo mawili ulianza kufanyika baada ya kutokea kwa janga hilo kwa misaada mbalimbali ya wadau na hadi sasa bweni moja limekamilika na la pili linaendelea na ujenzi wa paa.

“Hadi juzi hiyo zaidi ya Sh62 milioni zilikuwa zimepatikana kutoka kwa wanafunzi waliokuwa wamelipa fedha. Lakini mpango wetu kwa vile mabweni yaliyoungua tulishajiongeza awali kabisa kwa wadau, tunataka hizi fedha za wanafunzi zijenge mabweni mengine mapya ya kisasa kabisa,” alisema Mahundi.

Advertisement