RC Mghwira aziangukia familia hofu maambukizi ya corona Kilimanjaro

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amezitaka familia zilizopokea ndugu kutoka nchi jirani kupitia njia za panya na hawakukaa karantini kwa siku 14, kuwapeleka kwenye vituo vya afya ili kupimwa afya zao kama wana maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Rombo. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amezitaka familia zilizopokea ndugu kutoka nchi jirani kupitia njia za panya na hawakukaa karantini kwa siku 14, kuwapeleka kwenye vituo vya afya ili kupimwa afya zao kama wana maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

Rais  wa Tanzania, John Magufuli alitoa maagizo ya wanaoingia nchini kukaa karantini kwa muda huo kwa gharama zao lakini katika baadhi ya maeneo baadhi ya watu hukwepa kukaa karantini jambo linalohatarisha usalama wa watu wengine.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa agizo hilo leo Jumatatu Aprili 13, 2020 baada ya kutembelea na kukagua  mipaka wilayani Rombo na nchi jirani ya Kenya iliyopo Rongai, Kamwanga na Holili.

''Niziombe familia zote za Rombo ambako kuna mwingiliano na nchi jirani ya Kenya kama wana ndugu yako amekuja kutokea nchi jirani wampeleke akapime na akae siku 14 ili tuthibitishe hana maambukizi ya ugonjwa na hata kuambukiza wengine na kutupa ugumu wa kuwahudumia.”

“Lindeni afya zenu hakikisheni anayeingia ni mzima na salama na awe ametumia taratibu za afya. Akiingia msiyemtambua chukueni namba wapatieni maofisa waliopo karibu yenu. Nimemwagiza Mganga mfawidhi wa Wilaya ahakikishe hapa Rongai watu wote wanapimwa na nyie muwe wasimamizi wenyewe kwa wenyewe,” amesema Mghwira.