RC aagiza karantini zilindwe kuepusha wanaotoroka

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga

Kigoma. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo kuimarisha ulinzi katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya karantini kufuatia uwepo wa taarifa za baadhi ya watu waliotengwa kuonekana mtaani wakitafuta chakula.
Akizungumza leo Alhamisi Aprili 9, 2020 mjini Kigoma wakati wa ziara katika bandari ya Kibirizi ya usafirishaji mizigo kwa boti kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo nchi za  Congo na Burundi, Maganga amesema ugonjwa upo na kila mmoja anatakiwa achukue tahadhari.
Amesema taarifa zipo za wazi wazi kuwa watu waliwekwa karantini wanajichanganya mitaani jambo ambalo ni hatari kwa wakazi wa mkoa huo, hivyo ni vyema vyombo vya ulinzi na usalama vikachukua hatua za kuimarisha ulinzi.
"Taarifa tunazo za baadhi ya watu waliotengwa kutoka na kwenda kutafuta chakula mitaani hii ni hatari kwa mkoa wetu na nchi yetu, niwaombe kamati ya ulinzi na usalama iweze kuchukua nafasi yake kwenye hili," alisema Maganga.
Pia Maganga alikataa ombi la wasafirishaji wa maboti la kuwekewa sehemu ya kuhifadhiwa na badala yake wawekwe kwenye vyombo vyao vya usafirishaji vya majini kutokana na vyombo hivyo kutokuwa na huduma za muhimu kama choo na kuwepo uwezekano wa mabaharia kutoroka.