RIPOTI MAALUMU: Watoto wenye udumavu hatarini kuugua magonjwa sugu wakifikia utu uzima

Dar es Salaam. Kati ya changamoto zinazokabili watoto wengi ni udumavu.

Udumavu ni hali ya mtoto kuwa na kimo kifupi kuliko umri wake.

Unyonyeshaji usiozingatia kanuni bora, kama kutomlisha mtoto chakula chochote kwa miezi sita zaidi ya maziwa ya mama na kumpa lishe duni, huchangia watoto wengi kudumaa.

Utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) kuhusu lishe uliofanyika mwaka 2018, unaonyesha kuna asilimia 31.8 ya watoto waliodumaa.

Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Afya Duniani, Malengo ya lishe 2025, katika kila kundi la watoto watano wenye umri chini ya miaka mitano hapa nchini, kuna watoto wawili waliodumaa.

Kibaya zaidi ni kwamba, mikoa inayozalisha chakula kwa wingi hapa nchini kama Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliodumaa.

Mtaalamu wa Lishe kutoka Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef), Tuzie Edwin anasema asilimia 31.8 ya tatizo la udumavu inamaanisha kwamba kwenye kila watoto 100, takribani 32 wanakabiliwa na tatizo hilo.

Tuzie anasema kiafya watoto walio dumaa wanapokuwa watu wazima wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kuugua magonjwa sugu.

“Wanakuwa hatarini kupata magonjwa sugu kama moyo, saratani. Udumavu unawapa mzigo mkubwa wakiwa wakubwa,” anaeleza mtaalamu wa lishe wa Unicef, Tuzie.

Tuzie anasema kufikiri kwa mtu mwenye tatizo hilo, kuchambua mambo, kutafakari kwake na hata kuelewa kwake masomo darasani huathiriwa na udumavu.

Mtaalamu mwingine kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita), Deborah Essau mtoto anasema mtoto aliyedumaa hudumaa kiakili pia.

“Kuna wakati unaweza kumchapa na kumpa adhabu kali mtoto darasani ukadhani anafanya kusudi kutoelewa kile anachofundishwa, kumbe akili yake ilidumaa kwa kukosa lishe,” anasema Debora.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na Unicef kiwango cha udumavu wa asilimia 30 au juu ni kikubwa zaidi.

“Ukilinganisha na utafiti wa mwaka 2014, udumavu ulikuwa kwa asilimia 34 kwa hiyo utaona tunapunguza watoto walio dumaa lakini asilimia 32 ni kubwa sana,” anasema.

“Japo tumepunguza kutoka asiliia 34.7 mpaka 31, 2018, namba kamili ya watoto waliodumaa haijapungua. Tulikuwa na wastani wa watoto milioni mbili na sasa wamefikia milioni tatu kwa utafiti huu wa mwaka 2019,” anasema Tuzie.

Anasema madhara ya udumavu hayawezi kurekebishwa baada ya miaka miwili ya mwanzo.

Kabla ya kuzaliwa

Mtoto anaweza kuanza kudumaa kabla ya kuzaliwa wakati akiwa tumboni kwa mama yake.

Tuzie anasema ikiwa wakati wa ujauzito mama hatapata lishe bora, anaweza kusababisha mtoto kupata utapiamlo hata kabla hajazaliwa.

“Kwa mfano kama mama hatakula vyakula vya aina mbalimbali hasa vinavyoongeza damu wakati wa ujauzito, anaweza kumfanya mtoto akapata tatizo hilo,” anasema.

Tuzie anaeleza kuwa mama mjamzito anapaswa kuzingatia lishe bora na vidonge vya kuongeza damu ambavyo huwa wanapewa kliniki kwa ajili ya upungufu wa damu.

Tafiti nyingi zinaonyesha watoto wengi wanadumaa katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo ya maisha yao.

Mkunga wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Alphonsina Kaduma anasema akili ya mwanadamu huwa inatengenezwa ndani ya siku 1,000 za kwanza tangu azaliwe.

Anasema hiyo ina maana kwamba tumboni na miaka ya mwanzo ya ukuaji wa mtoto ndiyo kipindi muhimu cha kuzingatia masuala ya lishe kwa mtoto kuepuka udumavu.

Unyonyeshaji hafifu

Utafiti kuhusu lishe hali ya unyonyeshaji Tanzania kwa sasa ni asilimia 58.

Tuzie anasema zipo sababu zinazofanya kina mama wasinyonyeshe watoto wao ipasavyo na hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kupata utapiamlo.

Anataja baadhi ya sababu hizo kuwa ni mila na desturi potofu zinazowafanya wengi waanze kuwapatia chakula watoto kabla ya miezi sita ikiwa wataonekana kulia.

Anasema kikawaida mtoto anatakiwa anyonye ndani ya saa moja anapozaliwa.

“Baada ya hapo anyonye maziwa bila kitu chochote hata maji kwa miezi sita,” anasema.

Anaeleza kuwa baada ya miezi sita, mtoto anapaswa aanzishwe vyakula vya nyongeza huku akinyonya mpaka muda wa miaka miwili au zaidi.

“Kwa hiyo kuna ile hali ya kuwaza kwamba mtoto analia kwa sababu ya njaa anaamua kumpa uji au maji, Wamama kuna hali ya kuwaza mtoto anapolia anamaana kuna njaa,” anasema.

Anasema wakati mwingine mtoto anaweza kuwa analia kwa sababu ya joto baridi, anaumwa au tatizo jingine atapewa chakula.

Kwa asili ya wanawake wa Tanzania anakuwa na shughuli nyingi zaidi jambo linalomfanya ashindwe kumudu mwanae kunyonya kwa wakati.

Hali mbaya kwa wafanyakazi

Wanawake wanaofanya kazi wapo hatarini zaidi kushindwa kuwapa watoto wao maziwa pekee katika kipindi cha miezi sita ya awali.

Sheria za kazi zinataka mama akae nyumbani kwa miezi mitatu baada ya kujifungua kipindi ambacho mtoto anakuwa bado anajitaji maziwa.

Mama wa mtoto mmoja, Joyce Kudega anasema sheria hiyo inafuatwa zaidi kwenye mashirika ya umma na si binafsi.

“Mimi nilikaa nyumbani mwezi mmoja tu, mwezi wa pili nilianza kazi na nikawa namnyonyesha maziwa mtoto usiku hadi usiku. Ilibidi awe anakunywa uji,” anasema.

Tuzie anashauri mashirika, kampuni au taasisi kuwa na vyumba maalum kwa ajili ya unyonyeshaji

Kukacha kunyonyesha

Wakati wengine wakibanwa na mazingira kushindwa kunyonyesha watoto, wapo ambao wanakacha kulinda maumbile yao.

Nesi Kaduma anasema mtizamo huo ni finyu kwa sababu yanaandaliwa kwa ajili ya afya ya mtoto.

Anasema maziwa hayo yana virutubisho vyote muhimu na ni msaada mkubwa katika kujenga makuzi ya mtoto.

“Kwanza maziwa ya mama hayana gharama, yapo tayari wakati wote, ukinyonyesha unapunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti, niwashauri wanawake kuhakikisha watoto wao wananyonya” anasema Kaduma.

Anasema maziwa ya mama ni njia moja wapo ya uzazi wa mpango na yanajenga upendo baina ya mama na mtoto. Kinacho iponza mikoa yenye chakula Mkoa wa Iringa unaongoza kuwa na watoto wenye udumavu kwa asilimia 42.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda wakati akizundua ripoti ya utafiti huo mwaka huu aliishangaa mikoa yenye chakula kuathirika zaidi akisema udumavu ni vita kubwa nchini.

Mwananchi iliwahi kufanya utafiti mkoani Njombe na kubaini baadhi ya wazazi hupuuzia ulishaji wa watoto kutokana na kazi nyingi za shamba.

Baadhi ya familia zenye mifugo kama kuku, ng’ombe wa maziwa, mbogamboga na hata mazai ya nafaka zilikuwa na watoto wenye udumavu.

April 19, 2019 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Faustine Ndungulile wakati akijibu swali la Mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa bungeni, alisema tayari Serikali imechukua hatua kadhaa kukabiliana na udumavu.

Anasema baadhi ya hatua hizo ni kuandaa na kutekeleza mpango mkakati jumuishi wa kitaifa wa utekelezaji wa afua za lishe.

“Vigezo vilivyotumika kuangalia takwimu za lishe ni sampuli za kaya zilizo chaguliwa kushiriki kupitia utaratibu maalum wa kitaalamu,” anasema.

“Kwa kaya zilizochaguliwa watoto chini ya miaka mitano walipimwa urefu, kimo, uzito, wekundu wa damu pamoja na kuhoji maswali kwa mkuu wa kaya au mlezi kwa kutumia dodoso maalum.”