Rais Bashir ahaha kupata dhamana

Muktasari:

Dk Omar al Bashir anashtakiwa kwa tuhuma za kumiliki mabilioni ya fedha za kigeni kinyume cha sheria pamoja na kupokea zawadi katika njia isiyo rasmi.

Khartoum. Wakili wa Rais wa zamani wa Sudan, Omar al-Bashir amesema kuwa anatarajia kuwasilisha ombi la kutaka mteja wake aachiliwe kwa dhamana wakati kesi yake ya mashtaka ya rushwa ikiendelea.

Wakili Ahmed Ibrahim ambaye ndiye anamtetea kiongozi huyo wa zamani wa Sudan, amewaeleza waandishi wa habari leo Jumapili Agosti 25, 2019 kuwa ataiomba mahakama kumuwachia mteja wake kwa dhamana kwa sababu hiyo ni kesi ya kawaida.

Dk Bashir ameshitakiwa kwa tuhuma za za kumiliki mabilioni ya fedha za kigeni kinyume cha sheria pamoja nakupokea zawadi katika njia isiyo rasmi.

Wakati wa kusikilizwa kesi yake, jaji alitaka kupewa ombi la dhamana kupitia maandishi, akisema ofisi yake iko tayari kulipokea wakati wowote.

Ofisa wa polisi aliiambia mahakama Jumatatu kuwa Dk Bashir alikiri kupokea mamilioni ya dola kutoka kwa Saudi Arabia.

Hata hivyo, DK Bashir hakuzungumza chochote wakati kesi hiyo ilipofika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa.