Rais Dk Shein, Waziri Zungu wateta Ikulu Zanzibar

Muktasari:

Waziri Mussa Azzan Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala, aliteuliwa na Rais Magufuli Januari 23, 2020 kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Rais, Muungano na Mazingira huku aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene akiteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema miongoni mwa majukumu makubwa yanayopaswa kutekelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Azzan Zungu ni kulinda Muungano.

Amesema muungano huo utalindwa kama jitihada za waasisi wa Taifa hili, Hayati Abeid Amani Karume na Hayati Julius Nyerere walizozifanya zitaendelezwa na kudumishwa.

Dk Shein aliyasema hayo jana Ikulu mjini Zanzibar alipokuwa akizungumza na Waziri Zungu ambaye alimtembelea.

Alisema Serikali ya mapinduzi Zanzibar inamuhakikishia ushirikiano mkubwa anapotekeleza majukumu yake hasa yanayohusu muungano.

Zungu ameteuliwa hivi karibuni na Rais wa John Magufuli kuongoza wizara hiyo baada ya kufanya mabadiliko madogo ndani ya Baraza lake la Mawaziri.

“Mimi mwenyewe na viongozi wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Mawaziri wangu, tutahakikisha tunakupatia ushirikiano mkubwa kusudi utekeleze vema kazi zako,” alisema Dk Shein.

Alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta mafanikio makubwa kwa sababu walioungana ni wananchi wa pande mbili ambao wana udugu wa asili na historia ya muda mrefu.

Hivyo, alisema matarajio aliyonayo kutokana na utendaji kazi na uzoefu alionao Waziri Zungu ukiwamo uzoefu wa utumishi Serikalini  pamoja na ule wa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amehimiza mapenzi na udugu kwa wananchi wa pande mbili za Muungano uzidi kuimarishwa sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kihistoria.

Zungu amemshukuru Rais Magufuli na Dk Shein kwa uteuzi wake huku akiahidi kufanya kazi kwa niaba ya Watanzania wote.

Zungu aliyekuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Muungano, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, alimuhakikishia Rais Shein kuwa umoja mshikamano, upendo na udugu uliopo kati ya Serikali, wananchi wa Bara na Zanzibar unadumishwa na kuendelezwa kwa manufaa ya Tanzania.

Pia, alisema atahakikisha changamoto ndogondogo zinazowasumbua wananchi hususan wafanyabiashara, zinafanyiwa kazi na kumalizwa.

Alisema kuna changamoto nyingine husababishwa na baadhi ya watendaji.

Hivyo, aliahidi kuwa atahakikisha anaendeleza na kuzidisha  ushirikiano baina yake na viongozi wengine wa ngazi zote kusudi majukumu yake anayotekeleza yapate mafanikio kwa pande zote mbili za Muungano.