Rais Edgar Lungu akana kukandamiza wapinzani Zambia

Rais wa Zambia, Edgar Lungu

Lusaka. Rais wa Zambia, Edgar Lungu amekana kuwakandamiza viongozi wa upinzani nchini humo akisema mamlaka zinazowanyima vibali vya kukusanyika na kukutana na wafuasi wao zinafanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Polisi nchini humo wamekuwa wakitawanya mikutano ya wapinzani na wiki iliyopita walitumia mabomu ya machozi kutawanya mkutano wa Harry Kalaba katika Jimbo la Luapula.

Kalaba ni waziri wa zamani wa fedha katika Serikali ya Lungu, ambaye alijizulu mwaka jana akisema ni kuna ongezeko la vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa serikali.

Lungu alitetea kitendo cha polisi kuutawanya mkutano huo akisema “vyama haviwezi kufanya mikutano wakati wote tangu mwaka 2016 hadi 1921.”

“Ikiwa polisi wanaona si sahihi kufanya mkutano na wakazuia wapo sahihi kabisa,” Lungu aliwaeleza waandishi wa habari akiwa Ikulu.

Zambia imeendelea kuwa ya nchi ya amani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1991 uliomwondoa mwasisi wa taifa hilo Kenneth Kaunda.

Lungu alishinda uchaguzi wa mwaka 2016, ikiwa ni mwaka mmoja tangu awe rais wa nchi hiyo, baada ya kuchukua nafasi ya Michael Sata aliyefariki dunia mwaka 2014.

Tangu wakati huo amekuwa akilaumiwa kwa uongozi wa mabavu dhidi ya wapinzani wake.

Mshindani wake, Hakainde Hichilema aliyeshika nafasi ya pili katika uchaguzi wa 2016 na kukataa matokeo, alifungwa kwa miezi minne mwaka 2017 kwa madai ya kukataa kupisha msafara wa Rais Lungu.

Hali ya wasiwasi iliongezeka mwaka jana baada ya Rais huyo kushinda maombi yake katika mahakama ya Katiba, alipoitaka imruhusu kugombea tena.

Wapinzani na asasi za kiraia wanasema hiyo ni kukiuka Katika kwa kuwa Lungu akishinda tena mwaka 2021 atakuwa ametumikia vipindi vitatu – yaani mwaka mmoja aliomaliza kipindi cha Marehemu Sata, miaka mitano iliyofuata 2016-2021 na 2021-2026.