Rais John Magufuli aagiza upanuzi wa majengo ya hospitali ya wilaya Chato

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli hakufurahishwa na taarifa za viongozi wa halmashauri ya Chato kupoteza muda mwingi wakibishana juu ya upanuzi huo licha ya fedha za ujenzi kutolewa tangu mwezi Julai 2019, hivyo ameonya kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watu wakipata shida kwa uzembe wa viongozi wachache wa halmashauri

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, kuanza mara moja upanuzi wa majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa kuwa Serikali imeshatoa Sh1 bilioni kwa ajili ya ujenzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa Rais Magufuli hakufurahishwa na taarifa za viongozi wa halmashauri hiyo kupoteza muda mwingi wakibishana juu ya upanuzi huo licha ya fedha za ujenzi kutolewa tangu mwezi Julai 2019, hivyo ameonya kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watu wakipata shida kwa uzembe wa viongozi wachache wa halmashauri.

Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Eliud Mwaiteleke kuhakikisha ujenzi wa majengo hayo unafanyika na kwa gharama zinazostahili.

Aidha, Rais Magufuli amemtaka Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dk Ligobeth Kalisa kuhakikisha mashine ya X -ray inafanya kazi muda wote na wananchi wanapatiwa huduma kwa wakati.

“Sio sawa kwa Hospitali ya Wilaya kukosa huduma za x-ray, eti kwa sababu ya hakuna mikanda ya kupigia picha,” alisisitiza Rais Magufuli.

 

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 6 Desemba, 2019 alipowatembelea na kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato akiwamo Mzee Zephania Petro Kanoge ambaye ndiye aliyemhamasisha kuingia katika siasa mwaka 1995.

Mzee Kanoge na mwenzake marehemu Constantine Misungwi walimfuata Rais Magufuli mara mbili Jijini Mwanza alikokuwa akifanya kazi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza wakimtaka agombee Ubunge, licha ya kukataa wazee hao waling’anga’ania hadi alipokubali na wakabeba jukumu la kumfanyia kampeni kwa kutumia pikipiki hadi aliposhinda Uchaguzi Mkuu.

Rais Magufuli amemshukuru Mzee Kanoge kwa mchango wake mkubwa katika Maisha yake ya siasa na amemuombea apone haraka ili aweze kurejea nyumbani na kuungana na familia yake.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli amewaona wagonjwa wengine pamoja na wanawake na watoto waliofika kupata chanjo ambapo amewahakikishia kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuboresha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na hospitali mpya kote nchini, na kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh31 bilioni hadi kufikia Sh270 bilioni.

Rais Magufuli pia amekwenda eneo la Ginnery ambako ametoa pole kwa familia ya Mzee Mariganya Nghwenge aliyefariki dunia juzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu imeeleza kuwa Mzee Marigana anakumbukwa kwa ukulima wake hodari ambapo mwaka 1967 alizalisha mihogo mingi ukiwemo mhogo mkubwa alioutumia kumuonyesha Hayati Julius Kambarage Nyerere alipotembelea Chato na kuzungumza na wananchi.

Mjini Chato, Rais Magufuli amewasalimu wananchi waliokuwa wamesimama kando mwa barabara, na waliokuwa wakiendelea na biashara zao madukani ambapo wananchi hao wamemuombea, na kumpongeza kwa uongozi wake kumtakia heri katika majukumu yake.