Rais Kenyatta apunguza mshahara wake ili kupambana na corona

Wednesday March 25 2020Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Nairobi. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amepunguza mshahara wake na wa makamu wake William Ruto kwa asilimia 80 kwa ajili ya mapambano dhidi ya virusi vya corona huku mawaziri na makatibu wakuu wakipunguziwa asilimia 30.
Kenyatta ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa za maendeleo ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ambapo hadi kufikia leo wagonjwa walikuwa 28 huku mmoja akipona kabisa.
Kenyatta pia ametangaza kodi ya ongezeko la thamani kupungua kutoka asilimia 16 hadi 14 na amefuta kodi ya mapato kwa wafanyakazi wanaolipwa hadi kufikia Ksh24,000 (Sh 550,000 za kitanzania).
Katika mapambano ya kusambaa kwa virusi vya corona Kenyatta amesema kuanzia Machi 27, 2020 ni marufuku kutembea usiku kuanzia saa 1 jioni hadi saa 11 alfajiri kasoro kwa makundi machache maalum.
Makundi hayo yataainishwa na Waziri wa Afya ikiwa ni muendelezo wa hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kupambana na corona ambayo imesababisha wagonjwa zaidi ya 400,000 duniani.

Advertisement