Rais Magufuli, Mama Samia, viongozi mbalimbali walivyopokea kifo cha Bilionea Ali Mufuruki

Muktasari:

Mfanyabiashara Ali Mufuruki amefariki leo alfajiri alipokuwa akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini

Kufuatia kifo cha mfanyabiashara Ali Mufuruki  (60) kilichotokea leo Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu, Rais wa Tanzania,  John Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan, wametoa salamu zao za pole kwa msiba huo,

Kwa nyakati tofauti katika mtandao wa Twitter wameeleza walivyomfahamu mfanyabiashara huyo na kueleza walivyoguswa na kifo hicho.

“Nimehuzunishwa na taarifa za kifo cha rafiki yangu Ali Mufuruki (Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni - CEOrt). Nitamkumbuka kwa uzalendo na mchango wake katika kukuza sekta ya biashara na ushauri kwa Serikali. Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un” Ameandika Rais Magufuli katika mtandao wake wa Twitter.

Naye makamu wa Rais, Mama Samia ameandika, “Nimesikitishwa na taarifa ya kifo cha Ali Mufuruki. Allah ailaze roho yake mahala pema peponi. Sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea”

Mbali na viongozi hao wakubwa wa Taifa, viongozi wengine na wadau waliomfahamu Mufuruki wametumia mitandao yao ya kijamii kueleza masikitiko yao.

Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba ameandika, “Nimepoteza rafiki. Hakika kila nafsi itaonja umauti. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki. Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kuhimili maumivu ya msiba huu mkubwa. Mwenyezi Mungu ampe pepo marehemu.”

Kiongozi wa ACT Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe pia ameeleza katika mtandao wake namna alivyoguswa na kifo hicho cha Mufuruki.

“Sina maneno ya kusema zaidi ya kuwa sote ni wake Mwenyezi Mungu na kwake sote tutarejea. Sio tu alikuwa rafiki bali alikuwa mshauri wangu. Tulipishana mawazo fulani lakini alikuwa na heshima kubwa. Tangulia ndugu yangu  #RIPMufuruki.” Ameandika Zitto kabwe

Mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Hamad katika mtandao wake ameeleza masikitiko yake kwa kuandika “Nimepokea kwa huzuni, masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Ndugu Ali Mufuruki @amufuruki kilichotokea jana katika Hospitali ya Morningside, Johannesburg, nchini Afrika Kusini. Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi, Amin. Hakika sisi ni wa Mungu na kwake yeye tutarejea.”

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye katika mtandao wake wa Twitter amendika “Ni kazi ngumu sana kusimamia kile unachoamini hasa kama kitendo hicho kitakufanya msielewane na marafiki na watu wako wa karibu, LAKINI wewe Ally Mfuruki uliweza kuwa imara na mkweli kwa ulichoamini! Pumzika kwa amani!”

Kifo cha Mufuruki kimetokea leo huku ikielezwa kuwa alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Agakhan kwa takribani juma moja na hali yake ikabadilika jana, ndipo akasafirishwa kupelekwa Afrika Kusini na leo alfajiri ya Saa Tisa akafariki dunia.

Kwa mujibu wa Sanjar, mfanyabiashara huyo alikuwa akisumbuliwa na  ugonjwa wa homa ya mapafu (Nimonia).