Rais Magufuli abainisha dosari nchi za SADC, ataka mabadiliko

Muktasari:

Kabla ya kueleza ushauri wake kwa wafanyabiashara waliojitokeza kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC), Rais wa Tanzania, John Magufuli amesikitishwa na mchango mdogo wa biashara zinazofanyika ndani ya bara la Afrika, huku sehemu kubwa ya bidhaa zinazouzwa nje ya bara hilo zikiwa ghafi.

 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania John Maagufuli ametumia dakika 20 kueleza mambo sita yanayochagiza kukuza uchumi wa nchi za Afrika kupitia ushirikiano wa nchi za kusini mwa Afrika.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 Jijini Dar es Salaam, Tanzania wakati wa uzinduzi wa Maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC).

Katika uzinduzi huo utakaoanza leo hadi Alhamisi, Rais Magufuli ametumia lugha ya Kiswahili kati ya lugha nne za Kiingereza, Kireno, Kifaransa na Kiswahili zinazotumika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC), nchini Tanzania

“Tumekuwa waagiza wa bidhaa kutoka nje, ambazo zimekuwa na gharama kubwa. Pia nchi za Afrika zimekuwa wazalishaji wa nguvu kazi, wanaikimbia Afrika ili kwenda Ulaya na Marekani ili kufanya kazi huko, kwa hiyo tukizitumia fursa za ndani ya Afrika tutapiga hatua kubwa, ”amesema.

Chimbuko la wiki ya Viwanda ya SADC linatokana na maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa SADC uliofanyika  Aprili 29, 2015  mjini Harare, Zimbabwe.

Akitaja maeneo sita, ambayo ni ushauri kwa wafanyabiashara waliojitokeza kutoka nchi hizo za SADC, Rais Magufuli amewaambia washiriki jinsi anavyosikitishwa na mchango mdogo wa biashara zinazofanyika ndani ya bara la Afrika huku sehemu kubwa ya bidhaa zinazouzwa nje ya bara hilo zikiwa ghafi.

 

Kilichomshangaza zaidi ni namna wanunuzi wanavyotumia soko la Afrika, akisema asilimia 62 ya bidhaa zinazouzwa nje ya bara hilo ni ghafi huku nchi za Afrika zikijiwekea vikwazo katika biashara za ndani.

Rais Magufuli amesema Afrika imechelewa kimaendeleo, hivyo nchi wanachama wa SADC hawana budi kuanza kukimbia kwa vitendo.

“Inaifanya Afrika kubakia tegemezi, hii ndiyo gharama ya kutokuwa na viwanda, mapinduzi ya viwanda ndiyo njia ya lazima kuelekea mapinduzi ya kiuchumi,” amesema Rais Magufuli.

Amesema katika nchi za SADC zinatakiwa kuwekeza katika viwanda vidogo ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa watu wake, kuondoa vikwazo vya kibiashara, kuimarisha miundombinu inayounganisha nchi hizo.

“Tushughulikie vikwazo ndani ya SADC, tunawekeana vikwazo ambavyo havina maana yoyote, kuna utitiri mwingi wa kodi , hivi vyote tuviondoe,” amesema.

“Tuwekeze katika mazingira wezeshi ikiwamo umeme wa bei nafuu na uhakika, Tanzania tumeanza kuwekeza katika umeme wa mto Rufiji, ujenzi wa SGR baadaye utaunganishwa hadi Uganda, tunajenga bandari.”

“Pia tuhimize sekta binafsi katika kujenga viwanda, tuhimize, sekta binafsi ziache kulalamika, wanatakiwa kupigana na changamoto, hakuna cha bure bure, ndani ya SADC kuna fursa nyingi, madini kila mahali, kuna madini, kilimo, uvuvi na kadhalika, soko letu ni kubwa, zaidi ya watu milioni 350 , tuzichangamkie,” amesema