Rais Magufuli achangisha Sh35.1 milioni ujenzi wa bweni Mtama, awaonya watakaozila

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania John Magufuli amefanya harambee na kuchangisha kiasi cha Sh35.1 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bweni la shule ya Sekondari Mtama, baada ya bweni hilo kuungua kutokana na shoti ya umeme.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya harambee na kuchangisha kiasi cha Sh35.1 milioni ikiwa ni fedha za ujenzi wa bweni lililoungua katika Shule ya Sekondari Mtama mkoani Lindi.

Harambee hiyo ameifanya leo Jumanne Oktoba 15, 2019 aliposimama katika jimbo la Mtama wakati akienda wilaya ya Ruangwa ikiwa ni sehemu yake ya ziara mkoani Lindi.

Rais Magufuli alifanya harambee hiyo baada ya kupata taarifa kuwa bweni hilo liliungua baada ya kutokea kwa shoti ya umeme na kuamua kuchangisha fedha kwa viongozi mbalimbali aliokuwa ameambatana nao.

“Tunachangishana hapahapa sitaki suala hili nibaki nalo.”

 Amesema na kumuuliza Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ni kiasi gani cha fedha atakichangia ambapo alitaja Sh10 milioni. “Mheshimiwa Rais kwa kuwa fedha za jimbo zimekwisha ingia nitachangia Sh10 milioni,” amesema Nape.

Alipomuuliza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alisema, “Binafsi nitachangia Sh600,000 lakini kama Halmashauri itachangia Sh24 milioni.”

Rais Magufuli amesema yeye atachanga hapohapo.

“Mimi nachangia nisije toka jimbo la Nape bila kuchangia Sh5 milioni, nizitafute nizilipe hapahapa namkabidhi DC na Mheshimiwa Mbunge nimechangia kwa niaba ya mawaziri wote, mkuu wa mkoa na viongozi wote nilioongozana nao hizi fedha zikajenge mkiila mjue nanyi mmejila.”