Rais Magufuli achangisha papo hapo Sh1.4 milioni wanawake walioonewa, atoa maagizo

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amewachangisha viongozi fedha kwa ajili ya kuwapatia wananchi wanaotoa malalamiko mbele yake akidai ni moja ya kuwafanya viongozi hao wakumbuke kushughulikia matatizo ya wananchi maskini wanaowatumikia.

Kahama. Rais wa Tanzania, John Magufuli amelazimika kuwachangisha viongozi ngazi ya wilaya na Mkoa wa Shinyanga fedha kwa ajili ya kuwapatia wanawake wawili waliotoa kilio chao mbele yake wakidai kutotendewa haki na mamlaka za haki licha ya kuwasilisha vilio vyao kwao.

Wanawake hao ni Mariam Maricha na Neema ambao wametoa kilio chao leo Jumatano Novemba 27, 2019 wilayani Kahama mkoani Shinyanga wakati Rais Magufuli aliposimama kuwasalimia wananchi hao.

Mariam alimueleza Rais Magufuli kuna mtu mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Daudi alimpiga na kumvunja mkono lakini mtuhumiwa aliachiwa huru na polisi.

“Daud alinipiga akanivunja mkono, alikamatwa kupelekwa polisi, lakini nilipoenda siku inayofuata nilikuta ameachiwa hadi sasa sijui yupo wapi,” amesema Mariam ambaye mkono wake wa kulia ulionekana kufungwa bandeji maalumu

Baada ya kueleza hivyo, Rais Magufuli alimuita Mkuu wa mkoa huo, Zainabu Telack, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Kahama, Anderson Nsumba mbunge wa jimbo hilo (CCM), Jummne Kishimba, diwani na OCD ambapo zimepatikana jumla ya Sh500,000 na kumkabidhi mwanamke huyo.

“Nimewachangisha fedha hizi ili viongozi mliopewa dhamana mjue kushughulikia matatizo ya wananchi hawa maskini,” amesema Rais Magufuli

Naye, Neema amesema mumewe aligongwa na askari wa usalama barabarani akafariki dunia lakini licha ya kufuatilia amekuwa akizungushwa bila kupata msaada wowote.

Pamoja na kuchangisha Sh900,000 kwa ajili yake, kuhudumia watoto wake wawili, pia Rais Magufuli ameagiza askari huyo asimamishwe kazi pamoja na kufuatilia kesi hiyo ili mama huyo apate haki yake.

“Haiwezekani mwananchi wa kawaida akifanya kosa anafungwa hadi miaka saba lakini eti askari yeye hakamatwi yupo mitaani anazunguka na mnamuangalia, najua askari wanafanya kazi nzuri ila wapo wachache wanaoharibu,” amesema