Rais Magufuli ahimiza amani, mshikamano na kujitegemea sherehe za Uhuru

Muktasari:

Amani, mshikamano, kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea ni kati ya mambo yaliyosisitizwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika.

Mwanza. Amani, mshikamano, kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea ni kati ya mambo yaliyosisitizwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika mjini Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba leo Jumatatu Desemba 9, 2019, kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema Serikali imejipanga na itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kulinda amani na utulivu.

“Tumefanya mengi ya kujiletea maendeleo katika awamu zote kwa miaka 58 ya Uhuru lakini msingi mkuu wa mafanikio yote ni amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.”

“Serikali inawahakikishia wananchi kuendelea kulinda na kudumisha amani hiyo,” amesema Rais Magufuli.

Huku akitaja baadhi ya maeneo ambayo Taifa limepiga hatua ikiwemo kusomesha na kupata wataalam wa fani mbalimbali, kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, Rais Magufuli amesema amani, mshikamano na umoja wa Kitaifa ni nyenzo ya kufanikiwa zaidi.

“Kazi ya kuendeleza Taifa sio lelemama. Viongozi na waasisi wa Taifa hili wamefanya mengi kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto nyingi.”

“Ni jukumu letu kizazi cha sasa kuendeleza na kulinda yote mema yaliyoasisiwa na kusimamiwa na waasisi wetu,” amesema Rais Magufuli.

Ameongeza, “amani na usalama, umoja, mshikamano wa kitaifa, moyo wa kujitolewa na kujitegemea ni miongoni mwa nyenzo muhimu ya kutufikisha katika lengo la kuwa na Taifa lenye maendeleo endelevu.”

Mkuu huyo wa nchi ametumia fursa hiyo kujivunia mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, akitaja ujenzi wa viwanda zaidi ya 4,000, vita dhidi ya ufisadi, kudhibiti uvuvi haramu na ulinzi wa rasilimali za Taifa.

Magufuli ametaja maeneo mengine kuwa ni kuboresha usafirishaji kwa njia ya barabara, reli, maji na anga kwa kujenga miundombinu, kukarabati na kununua vyombo vya usafirishaji ikiwemo ndege, meli na mitambo.