VIDEO: Rais Magufuli ajitwisha deni la nyumba za JWTZ

Muktasari:

  • Rais John Magufuli amesema mkataba wa ujenzi wa nyumba uliosainiwa kati ya Serikali na kampuni ya Shanghai Construction Group ukiwataka askari wanaoishi kwenye nyumba zaidi 6000 ulikosewa na Serikali italibeba deni la zaidi ya Sh1 trilioni wanazodaiwa.

Dar es Salaam. Kufuatia ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo, Rais John Magufuli amesema wanajeshi hawatalipia nyumba zilizojengwa na kampuni ya Shanghai Construction Group ya China.

Awali, Jenerali Mabeyo amesema kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa na Serikali na kampuni hiyo, wanajeshi wanaoishi kwenye nyumba hizo zaidi ya 6000 nchi nzima wanakatwa kutoka kwenye Ngome Allowance.

Akizungumza leo Jumatatu Novemba 25, 2019 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa makao makuu ya JWTZ, Rais Magufuli amesema mkataba huo uliosainiwa mwaka 2013, Serikali inadaiwa zaidi ya Sh1 trilioni.

“Ukweli kabla sijaja hapa nimeshamwelekeza Waziri wa Fedha pamoja na Katibu mkuu na nafikiri kesho au kesho kutwa wataanza kulipia hilo deni ambalo limeiva. Tutaanza kulipia Dola zaidi ya 25 milioni na deni hilo ni kubwa zaidi ya Sh1 trilioni na kitu,” amesema Rais.

“Tulishazungumza na Waziri na leo CDF amesema hapa, huwezi ukamchukua askari ambaye anakaa kwenye maeneo ya kiaskari ni kama mahanga halafu uanze kumtoza pesa,” amesema

Amesema licha ya kuwa deni hilo ni kubwa lakini deni hilo litabebwa na Serikali ya Tanzania.

“Siwezi kuacha askari wangu kwenye utumwa wa nyumba za kulala. Badala ya kuota mabomu na namna ya kupiga risasi unaanza kuota namna ya kulipa deni ya nyumba. Kwa wakati huu hilo hapana,” amesema.

Amesema mkataba huo ulikosewa, lakini hawezi kukubali askari walipe katika kipindi chake.

“Kwa hiyo maaskari mnapoingia mahali kwenye nyumba zenu, lala salama, kama una mke wako lala salama, kama una mgeni amekutembelea lala salama, kama umekaribisha ndugu lala salama,” amesema huku akishangiliwa na Serikali.