Rais Magufuli ajivunia kununua ndege

Muktasari:

Rais John Magufuli ameeleza furaha yake kuhusu ununuzi wa ndege uliofanyika tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameeleza furaha yake kuhusu ununuzi wa ndege uliofanyika tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.

Ameeleza furaha yake hiyo leo Jumamosi Oktoba 26, 2019 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) muda mfupi baada ya kuongoza mamia ya Watanzania kupokea ndege ya mpya ya pili, Boeing 787-800 Dreamliner iliyowasili ikitokea nchini Marekani.

Magufuli amesema ndege hiyo ni ya saba kati ya ndege 11 zinazotarajiwa kununuliwa na Serikali ifikapo mwaka 2022.

“Kwangu ninajisikia vizuri kuwa kiongozi wa Tanzania, lakini najisikia vizuri kuwa mwenyekiti wa CCM. Haya yalizungumzwa kwenye ilani ya uchaguzi na sisi ni watekelezaji.”

“Hata nashangaa, Mungu anatupenda Tanzania. Wewe ndege kama hii inashuka hapa lazima tujiulize kwa nini haikushuka zamani? Huo ndiyo ukweli bila kuficha. Kwa nini ndege kama hii isubiri Magufuli ndio ishuke,” amesema Magufuli.

Huku akimshukuru Mungu, Rais Magufuli amesema mkakati wa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ni wa uhakika kulingana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.

“Waswahili husema ukitaka kwenda safari ndefu lazima uende na hatua fupi. Tulipoanza kuifufua ATCL na kuanza na ndege kubwa baadhi ya watu walidhani tuna beep, na wengine walipiga kejeli za chini.”

 “Nataka niwahakikishie kuwa shirika letu la ATCL linafufuliwa kama ilivyoelezwa kwenye ilani ya uchaguzi ya 2015.”

Awali akieleza mkakati wa miaka mitano wa ATCL, katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho amesema shirika hilo linatarajia kuwa na ndege mpya tisa zikiwemo ndege nne za  Bombardier Q400, ndege za masafa ya kati za Airbus A220-300 tatu na ndege mbili kubwa za masafa marefu ambazo ni Boeing 787 Dreamliner.