VIDEO: Rais Magufuli akerwa TBA kuchelewesha ujenzi hospitali Chamwino

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Novemba 22, 2019  amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuharakisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya Chamwino mkoani Dodoma na kukosoa ushauri uliotolewa na Wakala wa Majengo nchini (TBA)

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Novemba 22, 2019  amelitaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuharakisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya Chamwino mkoani Dodoma na kukosoa ushauri uliotolewa na Wakala wa Majengo nchini (TBA).

Ametoa kauli hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo utakaogharimu Sh3.4 bilioni  huku akimtaka Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Charles Mbuge kuwaweka mahabusu wataalamu wa TBA watakaochelewesha ujenzi huo.

“Hizi hela zimetoka siku nyingi maendeleo ya kazi hayaridhishi nasema kweli au uongo?” amehoji Magufuli huku akisema awali zilitolewa Dola 1000 za Marekani sawa na Sh2.4 bilioni huku Hazina kukiwa na salio la Sh995 milioni.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema awali ujenzi huo ulitolewa kwa TBA lakini walikuja na makisio ya Sh6 bilioni kiasi alichosema ni kikubwa kuliko makisio ya Serikali.

“Sasa hospitali za wilaya tunaweka Sh1.5 bilioni, hapa maana yake ni kama hospitali mbili na nusu. Vituo vya afya tunatumia Sh500 milioni na panakuwa na majengo matano hadi sita. Kwa nini hapa eneo moja iwe Sh6 bilioni.”

“Sasa kwa sababu mmenikaribisha kuweka jiwe la msingi na mimi mwenyewe niko hapa hata nikiwa nafanya mazoezi tutajuana vizuri. Kwa nini mlichelewesha ujenzi,” amesema Magufuli.

Amemuonya mkurugenzi wa TBA na kuhoji sababu ya jengo hilo kuwa na lifti wakati ni la ghorofa moja.

Mkurugenzi huyo alisema awali walikusudia kuweka lifti lakini akasema jambo hilo litatekelezwa fedha zitakapopatikana.

Kauli hiyo haikumridhisha Rais Magufuli, “sasa  katika jengo la ghorofa moja lazima uweke lifti? Kwa hiyo wewe unahitaji lifti au unahitaji hospitali ya kutibu wagonjwa.”

“Nisikilizeni wewe mkurugenzi pamoja na Brigedia Jenerali hawa wakiwachelewesha si una ma MP? Ukiona wanakuchelewesha weka ndani. Nataka jengo likamilike tunachelewa.”

Ametoa mfano wa nyumba za Serikali zilizojengwa eneo la Mbweni jijini Dar es Salaam akisema pia TBA walileta makisio yao aliyosema yangechelewesha ujenzi.

“Kule Mbweni wakaanza kutoa makisio  niliwazuia kwenda kule na nyumba zikajengwa mpaka leo zipo. Kwa hiyo wakianza kuwachelewesha msikubali. Kwa sababu hata jeshini kuna mainjinia, kwani mpaka mshauri wa ujenzi  atoke TBA,” amesema Magufuli.