Rais Magufuli akutana na Balozi wa China, umoja wa Ulaya

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli

akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) hapa

nchini Balozi Manfredo Fanti aliyeongozana na Balozi Emilio Rosetti

alipokutana naye Ikulu jijini Dar es salaam Februari 5, 2020

Muktasari:

Leo Jumatano Februari 5, 2020 Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya mazungumzo Ikulu ya Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (Sadc), Dk Stergomena Tax, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Manfred Fanti na Balozi wa China nchini humo, Wang Ke.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amekutana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (Sadc), Dk Stergomena Tax, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Manfred Fanti na Balozi wa China nchini humo, Wang Ke.

Baada ya mazungumzo yake leo Jumatano Februari 5, 2020 Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Sadc, Dk Tax amesema alikuja kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya jumuiya hiyo ikiwamo uendelezaji wa viwanda na kanda huru ya biashara ambapo wamekubaliana kuendelea kuhamasisha nchi wanachama kuendeleza viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

Ameelezea baadhi ya maeneo yaliyopo katika mkakati wa kukuza uchumi wa Sadc ni kuendeleza miundombinu hasa ya usafiri na nishati ambayo bado ni changamoto kwa nchi za Sadc lakini ameipongeza Tanzania kwa hatua madhubuti zinazoendelea kuchukuliwa ikiwamo ujenzi wa barabara, reli na kuongeza uzalishaji wa umeme.

Balozi wa EU

Kwa upande wake, Balozi wa EU nchini Tanzania, Manfred Fanti amesema mazungumzo yake na Rais Magufuli yamekuwa na manufaa makubwa ambapo wamejadili maendeleo mazuri ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na EU.

Amesema katika siku za karibuni wamekamilisha mazungumzo yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa EU kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania ambapo Sh132 bilioni zilizokuwa zimezuiwa zimeruhusiwa na sasa wanaandaa mpango mwingine wa miaka saba utakaoanza 2020.

Manfred Fanti amesema kwa jinsi anavyoyaona maendeleo ya Tanzania ana matumaini makubwa EU itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Tanzania ili kufanya vizuri zaidi.

Rais Magufuli amemshukuru Balozi Fanti kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na EU na amemhakikishia Tanzania itaendelea kushirikiana na EU katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande zote mbili.

 

 

Rais Magufuli

Aidha, Rais Magufuli amekutana na Balozi wa China nchini humo, Wang Ke na kumkabidhi barua aliyomwandikia Rais wa China, Xi Jinping akimpa pole kwa janga la homa ya virusi vya Corona lililolikumba Jiji la Wuhan nchini humo na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Pamoja na kukabidhi barua hiyo, Rais Magufuli amesema Tanzania imeguswa na kulipuka kwa janga hilo na ipo tayari kutoa ushirikiano wowote ambao Serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo.

“China ni ndugu zetu ni marafiki zetu, tunatoa pole kwa Rais Xi Jinping na Wachina wote waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia,” amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Balozi Wang Ke amemshukuru Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki kigumu.

Ametumia nafasi hiyo kueleza hali ilivyo nchini China ambapo amesema Serikali ya China imeanza kupata mafanikio katika kukabiliana na homa hiyo, imefanikiwa kuzuia isienee katika nchi zingine kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Aidha, amemhakikishia, Rais Magufuli kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na mtu yeyote aliyethibitika kuambukizwa homa ya Corona pia Watanzania 400 waliopo katika Jiji la Wuhan ambao wengi wao ni wanafunzi hawajaambukizwa homa hiyo na jitihada za kuhakikisha wanakuwa salama zinafanyika.