Rais Magufuli alivyozungumzia wanaobeza Mapinduzi ya Zanzibar

Muktasari:

Kesho Jumapili ya Januari 12, 2020 Zanzibar wanasherekea miaka 56 ya Mapinduzi ya Visiwa hivyo yaliyofanyika Januari 12 mwaka 1964.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema atahakikisha Mapinduzi ya Zanzibar yanaenziwa na kuahidi hakuna mtu wala kikundi cha watu watakaouchezea.

Rais ameyasema hayo leo Jumamosi, Januari 11, 2020 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa shule ya Mwanakwerekwe mjini Unguja, ikiwa ni sehemu ya shamra shamra ya kuadhimisha miaka 56 ya mapinduzi  ya Zanzibar  yaliyofanyika Januari 12, 1964 chini ya uongozi wa Abeid Amani Karume.

“Nitahakikisha Mapinduzi ya mwaka 1964 yanaendelea kudumu na hakuna mtu au kikundi cha watu kitakachochezea mapinduzi haya, ndiyo yameifanya nchi yetu iwe hapa, tuwe na amani.”

“Kumbukeni siku zote palipo na amani na utulivu mengi mazuri hufanyika tuendelee kutunza amani yetu,  palipo na amani uchumi wake hupanda juu, pana maendeleo, elimu itatolewa, utulivu upo na pana mungu pia kwa hiyo tuendelee kutunza amani yetu kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesema Rais Magufuli.

Aidha ametoa onyo kwa mkandarasi anayeendelea na ujenzi katika shule hiyo kwa kuwa alitakiwa amalize mwaka 2019 ujenzi huo, huku akimwagiza kuharakisha ujenzi kabla ya muda alioongezewa.

“Nimeshangaa katibu mkuu unawatetea hawa kwamba ni sababu za mvua unapochelewesha mradi mnachelewesha maendeleo,” amesema

“Lazima mguswe katika kufanya kazi mmeahidi Machi mtakamilisha ninataka kabla ya Machi 30 jengo liwe limekamilika na wanafunzi wanaingia ndani, hii fedha ni ya Watanzania Wazanzibar mtailipa mkandarasi asiwe kikwazo wanafunzi kusoma, ninataka umalize kwa wakati sitaki ucheleweshaji,” ameagiza.

Rais Magufuli amesema amekuwa akisitikishwa na matokeo ya wanafunzi yanapotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) na kuonyesha shule za Zanzibar zinakuwa za mwisho.

Amesema ni aibu ambayo viongozi wanapaswa kuifanyia kazi ili aibu hiyo iweze kuondoka.