Rais Magufuli amfukuza kazi mtumishi aliyechana Quran

Muktasari:

Februari 7, 2020 Waziri wa Tamisemi nchini Tanzania, Seleman Jafo alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kumsimamisha kazi Daniel Elimringi ambaye video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zilimuonyesha akikanyaga kitabu cha dini.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemfukuza kazi mfanyakazi wa halmashauri ya Kilosa mkoani Morogoro, Daniel Elimringi ambaye alichana kitabu kitakatifu cha Quran hadharani na kurekodiwa katika video fupi iliyosambaa kwenye mitandao.

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo Februari 11, 2020 jijini Dar es Salaam wakati akifungua jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni zilizopo katika eneo la Gezaulole.

Amesema Serikali haiwezi kuwa na watumishi wajinga kama kijana huyo, hivyo, ameondoa adhabu ya kusimamishwa aliyopewa na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo wakati suala hilo likichunguzwa.

“Juzi nilikuwa namsikia Mheshimiwa Jafo, mtu mmoja kule Kilosa alichana kitabu kitakatifu, nakushukuru umechukua hatua ya kumsimamisha kazi lakini mimi namfukuza kazi moja kwa moja.”

“Ashinde kesi asishinde huyo siyo mfanyakazi wa Serikali. Hatuwezi kukaa na wafanyakazi wapumbavu katika Serikali hii. Waziri umetimiza jukumu lako la kumsimamisha kazi, mimi namfukuza,” amesema Rais Magufuli katika hafla hiyo.

Rais Magufuli alimtaka Waziri Jafo kumwandikia barua kijana huyo kuhusu kufukuzwa kazi na kwamba akitoka huko mahabusu atajua mwenyewe atakavyoyatafuta maisha mengine.

Sakata la kijana huyo kuchana Quran lilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuibua gumzo huku baadhi ya watu wakitaka hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya kijana huyo kwa kudharau imani za watu.

Waziri Jafo alichukua hatua haraka kwa kutangaza kumsimamisha kazi kijana huyo wakati suala hilo likichunguzwa.