Rais Magufuli ampa onyo Waziri Mbarawa

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania John Magufuli amempa onyo Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akimtaka kuwachukulia hatua walioleta uzembe katika kuchelewesha mradi wa maji wilaya ya Masasi kabla hajamchukulia hatua yeye mwenyewe.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania John Magufuli amemtaka Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa kuwachukulia hatua waliokwamisha mradi wa maji wilayani Masasi mkoani Mtwara kabla hajamchukulia yeye hatua.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 16, 2019 wilayani Masasi ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Lindi. Ziara hiyo imeingia shubiri baada ya vituo anavyotembelea leo kukutana na changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Awali, alitaka kujua changamoto ambapo baadhi ya wananchi walitaja maji na umeme, hapohapo Rais Magufuli alimtaka Waziri Mbarawa kuzungumzia suala hilo na ndipo alipomtaja mhandisi kuwa anahusika.

Rais Magufuli alimwita mhandisi huyo na kutaka kujua sababu ya ucheleweshaji mradi huo ambaye alisema wamepewa kipindi cha miezi sita kufanya upembuzi yakinifu kabla ya kuanza mradi huo.

“Mkataba mmeuandaa ninyi, kwa nini muandae kwa miezi sita? Waziri nakupa wiki mbili nendeni mkaufute, hamuwezi kufanya upembuzi yakinifu miezi sita kujua suala moja la maji… ni shida kweli mnataka nizungumze mara ngapi nataka wiki mbili wamalize na waanze kujenga.”

“Wanadanganya nini hawa…Profesa Mbarawa nenda kalisimamie kama kuna mkataba mkaufute leo nataka maji yapatikane hapa Waziri nimeshakueleza, haya sikutakiwa kuzungumza hapa hadharani inaudhi,” amesema

“Utafukuzwa wewe…ninataka mambo yaende sawasawa fukuza hawa watu kabla hujafukuzwa wewe, hakuna haja ya kuchukua nje mainjinia kama mnao serikalini muwalete hapa mjenge wenyewe.”

“Nimeteuliwa na (Rais mstaafu Benjamin) Mkapa miaka 10 kuwa waziri kipindi chake chote, aliyenifundisha kazi mama Anna Abdalah anatoka hapa Masasi leo hii mnaleta mambo ya ajabu hapa.”

Mkapa alikuwa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 1995 hadi 2005 ambaye anatokea Masasi sawa na Mama Abdallah aliyewahi kuhudumu nafasi ya uwaziri anayetokea eneo hilo.