Rais Magufuli amtwanga Kitwanga mara mbili

Muktasari:

Rais Magufuli pamoja na Kitwanga wanaelezwa kuwa ni marafiki wa karibu wa muda mrefu hata kabla wawili hao hawajaingia kwenye siasa. Leo Rais Magufuli amefichua kwamba ana nasaba na Wilaya ya Misungwi kutokana na ndugu zake wa damu kuishi, kufariki na kuzikwa wilayani humo.

Mwanza. Mbunge wa Misungwi (CCM) mkoa wa Mwanza nchini Tanzania, Charles Kitwanga ni kati ya viongozi waliopata fursa ya kusalimia wananchi wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo Jumamosi Desemba 7, 2019, Kitwanga ametumia fursa hiyo kummwagia sifa ya ujasiri na uthubutu Rais wa Tanzania, John Magufuli kwa uamuzi wake wa kutumia fedha za ndani kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo.

Hata hivyo, sifa na pongezi hizo zilizoambatana na kufichua siri ya uthubutu wa Rais Magufuli kabla hajashika wadhifa huo hazikuweza kumwokoa Kitwanga na kitwango kutoka kwa mkuu huyo wa nchi.

Akihutubia wananchi, huku akitumia lugha mchanganyiko wa Kiswahili na Kisukuma, Rais Magufuli amemtwanga Kitwanga mara mbili katika hotuba yake fupi kabla ya kuweka jiwe la msingi.

Kwanza Kamtwanga kwa kutoketi jirani na mke wake na badala yake kukaa na mwanamke mwenye ngozi nyeupe.

“Nakupongeza Chifu Kapufi (kiongozi wa jadi Charles Kapufi) kwa kukaa jirani na mke wako tafauti na mheshimiwa Kitwanga; hebu mama Kitwanga simama watu wakuone,” amesema Rais Magufuli kwa utani huku yeye na hadhira inayomsikiliza wakiangua kicheko

Rais Magufuli akasema, “wanawake weupe hoyeeee.” Hali iliyoibua furaha kwa washiriki wa hafla hiyo

Kama vile haitoshi, Rais Magufuli akamtwanga Kitwanga kwa mara nyingine pale alipogoma mwaliko wa kwenda Msungwi kutatua matatizo na migogoro anayosema iko ndani ya uwezo wa viongozi wa kisiasa na Kiserikali Wilaya ya Misungwi na mkoa wa Mwanza.

“Hii migogoro midogo midogo ishughulikiwe na viongozi wa maeneo husika wakiwemo wabunge, wakuu wa Wilaya na mikoa pamoja na viongozi wa CCM,” amesema Rais Magufuli

Awali, akisalimia wananchi wakati wa hafla hiyo, Kitwanga ambaye pia ni maarufu kwa jina la ‘Mawe Matatu’ amefichua siri ya uthubutu wa Rais Magufuli kuhusu ujenzi wa daraja la Mkapa wakati huo akiwa Naibu ba baadaye Waziri.

“Nakumbuka tuliomba fedha kutoka Kuwait lakini walipopelekewa maombi ya malipo ya awali ya dola 1 milioni wakaweka sharti la kulipwa kwanza deni la dola 10 milioni. Nakumbuka ulisema kama tunazo fedha hizo si ni bora kuzitumia kumlipa mkandarasi moja kwa moja,” amesema Kitwanga

Mbunge ambaye hakutaka kuingia kwa undani kuhusu siri za uthubutu wa Rais Magufuli anazozifahamu pia ametaja jinsi kiongozi huyo alivyofanikiwa kumshawishi Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa kuhusu kutumia fedha za ndani kujenga mtandao wa barabara kuunganisha mikoa yote ya Tanzania.

“Leo hii inaweka jiwe la msingi kujenga daraja lenye urefu mara tatu zaidi ya lile la Mkapa. Nisiseme mengi; itoshe tu kusema nina furaha sana na Mungu akulinde, akuongezee maisha marefu na afya njema. Sisi Misungwi tunasema tutakufia,” amesema Kitwanga

Katika kuhitimisha hotuba yake, Kitwanga akatumia fursa hiyo kumwomba na kumwalika Rais Magufuli kutembelea wilaya ya Misungwi akisema ni ombi alilopewa na wazee wa Misungwi kuliwasilisha kwa mkuu huyo wa nchi.