VIDEO: Rais Magufuli apongezwa kusimamia upatikanaji wa umeme Tanzania

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa Tanzania imekuwa nchi mojawapo yenye uhakika wa nishati ya umeme baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo nchini humo tangu alipoingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015.

Dar es Salaam. Waziri wa biashara na viwanda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  Amina Salum Ally amesema Tanzania imekuwa nchi mojawapo yenye uhakika wa nishati ya umeme baada ya Rais wa Tanzania John Magufuli kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo.

Waziri Amina ameyasema hayo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 wakati akiwasilisha mada katika uzinduzi wa maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda kwa nchi 16 wanachama wa SADC.

Amesema Tanzania kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo, utawezesha ukuaji wa viwanda vya uzalishaji bidhaa mbalimbali kwa ufanisi.

"Mafanikio haya si ya Tanzania pekee bali nishati hii itasaidia katika zingine pia za SADC, Serikali ya Tanzania imeweza kujenga bwawa kubwa ili kujihakikishia uwepo wa umeme wa uhakika, uwepo wa nishati wa Afrika nzima na mpaka hapa Tanzania ya viwanda inawezekana," amesema.

Wakati huohuo Katibu Mtendaji wa SADC, Dk Stegomena Tax, amesema Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa SADC kwa mwaka mmoja utawezesha vikao zaidi ya 30 kufanyika Tanzania.

"Kutakuwa na majadiliano mbalimbali, uendelezwaji wa fursa ya miondombinu utaweza kuunganisha na pia fursa ya kujenga ushirikiano kati ya wafanyabiashara wa nchi 16 za SADC," amesema Dk Tax.