VIDEO:Rais Magufuli atamani kuona mabilionea wengi Tanzania

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais John Magufuli amesema anatamani siku akimaliza muda wake wa uongozi Tanzania kuwepo na wafanyabiashara mabilionea zaidi ya 100 na kuwataka kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo za biashara


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema anatamani anapomaliza muda wake Tanzania iwe na mabilionea zaidi ya 100.

Ameyasema hayo leo Juni 7, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano baina yake na wafanyabiashara kutoka wilaya zote Tanzania  kujadili changamoto zinazokwamisha sekta hiyo.

Kikao hicho kimehudhuria pia na watendaji mbalimbali wa Serikali ya Tanzania wakiwamo mawaziri na wakuu wa vyombo vya dola.

Magufuli amesema suala hilo litamfanya afurahi kuwa anamaliza muda wake na kuacha mabilionea wengi katika nchi kutokana na kile alichokuwa akikifanya katika kuboresha mazingira ya biashara.

“Thubutuni na msiogope kufanya biashara ya aina yoyote, nchi yetu imebarikiwa kuwa na ardhi nzuri, rutuba, maji kwa ajili ya uvuvi, mifugo, madini fursa nyingi za uwekezaji zitumieni ili ziwanufaishe ili siku nikiwa naondoka angalau niache wafanyabiashara mabilionea zaidi ya 100 nitafurahi sana.”

"Biashara mipakani kwetu Watanzania bado iko chini, tutumie fursa ya masoko ya Afrika ya Mashariki na SADC ili tuweze kwenda mbali kwa sababu masoko haya yanaunganisha mamilioni ya watu,” amesema

Magufuli amesema, “Semeni yale yote ambayo mnaona ni kero kwenu na mnataka tuyafanyie kazi, msiogope na kila mmoja azungumze kadri anavyoona kwa faida.”

Kiongozi huyo aliyeingia madarakani Novemba 5, 2015 atahitimisha muhula wa kwanza wa miaka mitano mwaka 2020 na endapo akichanguliwa tena ataongoza muhula wa pili na mwisho hadi 2025 kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.