Rais Magufuli ateua wenyeviti watano wa bodi, yumo Mrema wa TLP

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Tanzania imesema Rais John Magufuli ameteua wenyeviti watano wa bodi akiwamo Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha TLP, Agustino Mrema.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amefanya uteuzi wa wenyeviti watano wa bodi za taasisi za Serikali baada ya bodi za taasisi hizo kumaliza muda wake.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa leo Jumatatu Januari 20, 2020 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imesema wenyeviti hao wameongezewa muda baada ya vipindi vyao vya awali kumalizika;

Kwanza, Rais Magufuli amemteua Agustino Mrema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.  Pia, Mrema ni mwenyekiti wa chama cha siasa cha upinzani cha TLP.

Pili, Rais Magufuli amemteua Dk Harun Ramadhani Kondo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Uteuzi wa Mrema na Dk Kondo umeanza Januari 20,  2020.

Tatu, Rais Magufuli amemteua Profesa Mayunga Habibu Hemed Nkunya kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).

Nne, Rais Magufuli amemteua Fidelis Mutakyamilwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Taifa Mipango na Matumizi ya Ardhi.

Tano, Rais Magufuli amemteua Peter Maduki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Uteuzi wa Profesa Nkunya, Mutakyamilwa na Maduki umeanza Januari 17, 2020.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Dk Noel Logwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa. Uteuzi wa Dk Logwa umeanza Januari 17, 2020 na kabla ya uteuzi huo alikuwa Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Akiolojia na Mafunzo ya Urithi (Archeology and Heritage Studies) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Dk Logwa amechukua nafasi ya Profesa Audax Mabula ambaye amestaafu.