VIDEO: Rais Magufuli atoa maagizo kwa DED wa Dodoma, meneja wa Tanroads

Muktasari:

Rais John Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) jijini Dodoma na kuagiza wananchi wanaoishi katika sehemu ya eneo hilo kulipwa fidia kuanzia Desemba Mosi mwaka huu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma (DED), Godwin Kunambi kuanza kuwalipa wananchi fidia zao Desemba Mosi, 2019 ili kupisha ujenzi wa Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 25, 2019 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa makao makuu ya JWTZ yatakayojengwa katika eneo la Kikombo jijini humo ikiwa ni mwendelezo wa serikali kuhamia Dodoma.

Amemtaka Mkurugenzi wa Jiji kubeba jukumu la kuwalipa wananchi 1500 wanaoondolewa kwenye eneo hilo jumla ya Sh3.399 bilioni kwa sababu jiji hilo litanufaika kwa JWTZ kuhamia Dodoma na wananchi hao pia ni wakazi wa Dodoma.

“Ninatoa maelekezo leo kwa mkurugenzi wa jiji, achukue hizo Sh3.399 bilioni, kuanzia Desemba Mosi aanza kuwalipa fidia wananchi wa hapa,” amesema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wanajeshi pamoja na wananchi waliohudhuria hafla hiyo.

Rais Magufuli amewataka pia wananchi wa maeneo hayo kuzitumia vizuri fedha watakazozipata kwa kununua ardhi katika maeneo mengine na kujenga nyumba za kisasa. Amewahakikishia kuwa wote wanaostahili watalipwa fidia kuanzia Disemba Mosi.

Amewataka pia mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, mkuu wa wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi  pamoja na katibu tarafa kuanza kusaini nyaraka za watu wanaostahili mapema ili malipo yaanze kutolewa haraka ifikapo Disemba Mosi.

“Nataka nitoe wito kwa wananchi mnaostahili kupiwa fidia, msianze kubadilisha fidia. Nafahamu wameshaanza kujitokeza matapeli, wengine wanapita kwenye maeneo yenu, wengine wanajiita ni wenyeviti wa kutetea wananchi kupata fidia, wengine mnawachangia mpaka hela ili wakawatetee. Hao matapeli achaneni nao,” amesema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemuagiza meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoa wa Dodoma kuhakikisha kipande cha barabara ya kilomita 18 kinachopita kwenye eneo hilo kinajengwa kwa lami na kuanzia wiki ijayo ahakikishe anatangaza zabuni ya wakandarasi.