Rais Magufuli atoa onyo zito kwa mameneja Tanroads

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema mkoa ambao barabara au daraja litakatika Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), atakuwa hana kazi.
Ameyazungumza hayo leo wakati akikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara nane Mbezi jijini hapa ambazo mkandarasi alisema zitamalizika Oktoba mwaka huu.
Rais Magufuli amesema fedha za kufanya ukarabati zipo katika ofisi za Tanroad mikoa yote.
“Natoa wito kwa Tanroad sitaki kuona barabara ya mkoa au barabara kuu imejifunga kisa daraja limekatika hiko sitaki kusikia nimeona niwape tahadhari mapema,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesisitiza kuwa “ngoja niende huko Morogoro nasikia kuna daraja limewashinda huko Morogoro.”
Magufuli amewapongeza Tanroad mkoani hapa kwa kutengeneza barabara mbalimbali zikiwemo za mtaani na kumpandisha aliyekuwa anakaimu nafasi ya Meneja Mkoa Tanroad, Mhandisi Ngusa Julius kwa mwaka mmoja na kuwa meneja rasmi.
Vilevile, Rais Magufuli amesema sababu ya kujengwa barabara nane ni baada ya kukosa fedha ya wafadhili kutokana na masharti na wakatenga Sh140 bilioni.
“Mnapoona tunapowabana mafisadi msiwaoonee huruma maana yake tunarudisha fedha walizochukua kwa wananchi,” amesema Magufuli.