VIDEO: Rais Magufuli atoa salamu za Krismasi akigusia mambo matano

Sunday December 22 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa salamu za Krismasi na mwaka mpya 2020 huku akigusia mambo matano.

Mambo hayo ni amani, upendo, mafanikio, maendeleo na kujenga umoja.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa salamu zake leo Jumapili Desemba 22, 2019 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria wilayani Chato Mkoa wa Geita aliposali dominika ya nne ya majilio.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Magufuli amesema tunapoelekea katika sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya, wakristo na waumini wa madhehebu mengine wana  jukumu la kuendelea kuombea amani, upendo na umoja kwa wanadamu wote bila kubaguana.

“Niwaombe ndugu zangu wa Chato na Watanzania kwa ujumla, tusherehekee sikukuu ya Krismasi kwa amani na upendo mkubwa.”

“Lakini pia tuukaribishe mwaka mpya kwa amani na upendo mkubwa wa kristo, mwaka unaokuja uwe mwaka wa mafanikio, uwe mwaka wa maendeleo, uwe mwaka wa kujenga umoja wetu kwa Watanzania wote, uwe mwaka wa amani na upendo na uwe mwaka wa kuendeleza Taifa letu katika maendeleo ya kweli,” amesema Rais Magufuli.

Advertisement

Amewapongeza waumini wa parokia hiyo kwa kazi kubwa ya upanuzi wa kanisa wanayoendelea nayo. Magufuli alichangia fedha mwaka 2016 kwa ajili ya upanuzi wa kanisa hilo.

Misa ya leo imeongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Henry Mulinganisa.


Advertisement