Rais Magufuli atuma salamu za rambirambi kifo cha Arap Moi

Muktasari:

Rais wa awamu ya pili wa Kenya, Daniel Arap Moi aliyezaliwa Septemba 2, mwaka 1924, katika jamii ya wakulima katika eneo la Baringo, magharibi mwa Kenya amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne Februari 4, 2020 katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa niaba ya Watanzania kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa pili wa nchi hiyo, Daniel Arap Moi (95).

Moi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne Februari 4, 2020 katika Hospitali ya Nairobi, Kenya alikokuwa anapatiwa matibabu.

Rais Magufuli ametumia akaunti yake ya Twitter kutuma salamu hizo akisema, “kwa niaba ya Serikali na Watanzania nakupa pole Mhe. Rais Uhuru Kenyatta na Wakenya wote kwa kuondokewa na Rais mstaafu Daniel Toroitich arap Moi.”

“Watanzania tutamkumbuka kwa uongozi wake mahiri, jitihada za kuimarisha uhusiano wetu na Kenya na kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki,” ameandika Rais Magufuli

Mwili wa Moi tayari ushatolewa Hospitali ya Nairobi na kupelekwa eneo la kutoa huduma za mazishi la Lee ambalo ni maarufu nchini humo.

Daniel Arap Moi jina lake la kwanza lilikuwa Toroiticha arap (mwana wa) Moi lakini baadaye akabatizwa katika Ukristo na kupewa jina la Daniel wakati huo akiwa mwanafunzi.

Moi aliyeshika urais wa Kenya kati ya mwaka 1978 hadi 2002, alikuwa mmoja wa mwanasiasa mashuhuri waliofanikiwa, akitoka jamii ndogo ya Tugen, mojawapo ya makundi yanayounganisha kabila kubwa la Wakalenjin.

Alianza kufanya kazi kama mwalimu mwaka wa 1945 katika shule ya African Government School na mwaka mmoja baadaye akiwa na umri wa miaka 22 akateuliwa kuwa mwalimu mkuu.

Machi 1957 Moi alikuwa mmoja wa watu weusi wanane waliochaguliwa kuwa wanachama wa Bunge la Ukoloni ambalo kwa kifupi lilifahamika kama LegCo.

Mapema mwaka 1960 alikuwa mmoja wa wajumbe walioteuliwa kuhudhuria mkutano katika Lancaster House jijini London, ambapo Katiba mpya iliandaliwa na kuwapa Waafrika viti vingi katika Bunge.

Mwaka 1961 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, na katika baraza la mawaziri la muungano wa vyama vya kisiasa vilivyoshirikisha Kanu (Kenya African National Union), Kadu (Kenya African Democratic Union - chama cha Moi) baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.

Kenya baadaye ilipata Uhuru mwaka 1963 na Jomo Kenyatta akawa Waziri Mkuu, naye Moi akateuliwa kuwa Waziri kivuli wa kilimo katika muungano wa upinzani. Siasa za Kadu zilidorora kisha chama hicho kikavunjwa.

Akiwa madarakani, miongoni mwa mabadiliko aliyofanya ni kurejesha vyama vingi vya kisiasa lakini akatumia ujanja wa kuyagawa makabila mbalimbali nchini na kushinda uchaguzi miaka ya 1992 na 1997.

Hata hivyo utawala wa Moi ulidumaa kiuchumi na Serikali yake ilishutumiwa kwa ufisadi na hivyo Shirika la Fedha duniani (IMF) na Benki ya dunia (WB) walikataa kutoa mikopo kwa Kenya.

Katika Uchaguzi wa 2002 Moi hakugombea kwa kuwa alikuwa anazuiwa kushiriki kikatiba, hata alipojaribu kumwachia nafasi hiyo Uhuru Kenyatta, alishindwa vibaya na huo ukawa ndio mwanzo wa mwisho wa chama cha Kanu.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi