Rais Magufuli awapa siku tano Waziri Kigwangalla, Katibu wake kujirekebisha lasivyo atawafukuza kazi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amekuwa Rais wa kwanza wa Taifa hilo kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita akiwa madarakani. Akiwa katika kisiwa hicho amezungumza masuala mbalimbali ikiwamo kwa wateule wake wa wizara ya maliasili na utalii kuelewana lasivyo atatengua uteuzi wao.

Rubondo. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa siku tano  kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo atatengua uteuzi wao.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo Jumanne Desemba 31, 2019 alipokuwa akizungumza na maofisa na askari wanyamapori na Hifadhi ya Misitu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo ambako ametembelea na kujionea vivutio vya utalii.

Katika salamu zake, Rais Magufuli amelipongeza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kwa kazi nzuri ya uhifadhi, kukuza utalii na kuchangia mapato ya Serikali lakini ameelezea kusikitishwa kwake na mahusiano mabaya yaliyopo kati ya Waziri Kigwangalla na Profesa Mkenda hali ambayo inasababisha baadhi ya shughuli za wizara kusuasua.

“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, katibu mkuu na waziri kila siku wanagombana na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa.”

“Hilo ni lazima nilizungumze kwa dhati, siwezi kuwa na watendaji wa kuteua mimi halafu kila siku wanagombana, kuna mambo mengi hayaendi, Katibu Mkuu hamheshimu Waziri na Waziri naye hataki kwenda na Katibu Mkuu, siwezi kuvumilia hilo,” amesema Rais Magufuli

“Kwa hiyo nalizungumza hili siku ya leo tarehe 31 ya mwezi wa 12 (2019) kwamba wajirekebishe na ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku tano, wawe wanasalimiana, wanazungumza, mimi ninafahamu nina vyombo ninajua nani hafai zaidi,” amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ameiongezea muda Bodi ya Tanapa iliyomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti Jenerali Mstaafu George Waitara kutokana na kuridhishwa na kazi nzuri zilizofanywa na Tanapa chini ya uongozi wa bodi hiyo ikiwemo kuunda Jeshi Usu la Askari Wanyamapori na Hifadhi ya Misitu, na ametaka Tanapa iendelee kupiga hatua kwa maslahi ya Taifa.

Rais Magufuli amesema Tanzania yenye Hifadhi za Taifa 22, imetoa zaidi ya asilimia 32.5 ya eneo la ardhi yake kwa ajili ya hifadhi na kwamba imefanya hivyo kwa maslahi ya Watanzania na watu wote duniani wanaotembelea hifadhi hizo.

Amempongeza Kamishna wa Uhifadhiwa Tabapa, Dk Allan Kijazi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick Mofulu kwa kazi nzuri ya kudhibiti ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo, kutunza mazalia ya samaki na ndege ambao husafiri kutoka nchi mbalimbali duniani na kutunza uoto na wanyama mbalimbali waliomo katika hifadhi hiyo.

Ameahidi Serikali itatoa Sh2 bilioni kwa ajili ya kununua kivuko chenye uwezo wa kuchukua watu 100 na magari 4 ili kurahisisha usafirishaji wa watalii wanaoingia na kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Rubondo wakiwa na magari yao.

Rais Magufuli amesema kwa sasa Tanzania ina bustani za wanyamapori (zoo) 23, mashamba ya Wanyama 20 na ranchi sita na ametoa wito kwa Watanzania wakiwamo wastaafu katika tasnia ya wanyamapori kujitokeza kuanzisha bustani za wanyamapori, mashamba ya wanyama na ranchi ambazo zitasaidia kuvutia watalii na kuongeza kipato.

Mapema akimkaribisha Rais Magufuli, Kamishna Kijazi amemshukuru kwa juhudi zake za kutilia mkazo shughuli za uhifadhi na kupanua maeneo ya uhifadhi kutoka hifadhi 16 mwaka 2015/2016 hadi kufikia hifadhi 22 hivi sasa na ameahidi kuwa Tanapa itahakikisha hifadhi hizo zinatunzwa kwa manufaa ya Taifa.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo Kamishna Msaidizi Mofulu amesema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 456.6 inao Wanyama mbalimbali wakiwemo Sokwe, Pongwe, Swala, Tembo, Twiga na pia ni mazalia ya samaki wa ziwa Victoria na ndege mbalimbali, na kwamba katika kipindi cha kuanzia mwaka 2014/15 hadi 2018/19 idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo imeongezeka hadi kufikia 5,700 kwa mwaka, walioingiza shilingi Bilioni 1.4 katika pato la Taifa.