Rais Magufuli awatoa hofu wakuu wa mikoa, wilaya

Muktasari:

Rais John Magufuli amesema hatawabadilisha kwenye nafasi zao laini atafanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema hatarajii kufanya mabadiliko kwenye nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya hivyo amewataka watendaji hao wa Serikali waendelee kuchapa kazi.

Amesema atafanya mabadiliko kwenye Baraza la  Mawaziri akibainisha kuwa wapo ambao watarudi kwenye Baraza lake jipya katika awamu hii na wapo ambao hatawateua

Amesema hayo leo Jumatatu Novemba 09, 2020 wakati akimuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Profefa Adelardius Kilangi katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Mkuu huyo wa nchi amesema pamekuwa na tabia kila Serikali mpya ikiingia watendaji wanakuwa na hofu kwamba patatokea mabadiliko hivyo amewataka wateule wake kuendelea kuchapa kazi.

“Kwa sasa hivi wana hofu sana wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya na ninawashangaa kwa nini wanakuwa na hofu kwa sababu kama ni mafanikio ya Serikali ni pamoja na wao,” amesema.

“Mkuu wa mkoa unakuwa na wasiwasi gani, labda kama utendaji wako haukuwa vizuri, kwa sababu nashangaa napata vimeseji vingine, ‘mheshimiwa, Rais nimejitahidi katika kipindi changu’ kana kwamba nilimwambia kipindi chake kinaisha baada ya mimi kuapishwa,” amesema Rais Magufuli huku akicheka

“Nimeona hili nilizungumze kwamba wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya msiwe na wasiwasi na inawezekana wala pasitokee badiliko hata moja labda kwa mtu atakayestaafu au atakayefanya mambo ya hovyo sana.

“Kwa nini nibadilishe mkuu wa mkoa,” ameongeza.

Amewahakikishia wateule wake hao kuwa wataendelea kuwepo kwa kuwa alianza nao kazi na anategemea kumaliza nao.

“Najua inawezekana wananisikia, wachape kazi, wasipochapa kazi shauri yao, labda waandike barua ya kuondoka lakini najua nilianza nao. Wakuu wa mikoa, makatibu tawala, wakuu wa wilaya, Wakurugenzi, makatibu tawala na wengine katika maeneo mbalimbali wachape kazi hakuna cha kuwa na wasiwasi,” amesema.

Ameeleza kuwa eneo ambalo atafanya mabadiliko ni kwa mawaziri.

“Mabadiliko yatakayokuwepo ni kwenye mawaziri, kuna ambao watarudi na kuna ambao hawatarudi hili sitaki kusema uongo, nikishamaliza hilo basi wengine wachape kazi tu,” amesema Rais Magufuli.