VIDEO: Rais Magufuli awazungumzia wanaokiri uhujumu uchumi

Muktasari:

Rais Magufuli alitoa ushauri wa kuwasamehe watuhumiwa wa uhujumu uchumi watakaoandika barua ya kukiri tuhuma hizo wakati wa kuwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu ya Dar es Salaam, Septemba 22, 2019

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapongeza watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi waliokiri na kuwa tayari kurejesha fedha wanazotuhumiwa kuhujumu akisema amewasamehe moja kwa moja.

Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 30, 2019 Ikulu Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa Septemba 22, 2019 wa kuwasamehe watuhumiwa wa uhujumu uchumi watakaokiri makosa yao na kulipa kiasi cha fedha wanachotuhumiwa.

Katika taarifa ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) nchini humo, Biswalo Mganga amesema watuhumiwa 467 wameshajitokeza kuomba msamaha wakiahiri kurejesha zaidi ya Sh107 bilioni.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli amesema ameongeza siku saba kwa watuhumiwa wengine zaidi kujitokeza huku akisema msamaha wake ni wa kweli.

“Niwapongeze hawa 467 ambao documents (nyaraka) zao mmezichambua. Mimi naomba ofisi ya DPP mharakishe hizo process (mchakato), watu waanze kuwa free (huru), waanze kutoka, wakajumuike na familia zao,” amesema Rais Magufuli.  

Ameitaka ofisi ya DPP kuharakisha mchakato kwa waliojitokeza ikishirikiana na taasisi nyinginezo kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Magereza na Jeshi la Polisi.

“Isije tena ikawa hawa 467 mtakapochambua labda mkakuta wamebaki labda 400 au 300, kadhalika wakawa tena wanasubiri. Ilikuwa wiki mwishowe wiki mbili, mara mwezi mara mwaka, dhana ya msahama huu haitakuwa na maana,” amesema.

Ametoa wito kwa Watanzania wote na wenye tuhuma za uhujumu uchumi ambao wana nia ya kutaka kutubu na kurejesha hicho na kukiri makosa yao.

“Wala wasiwe na wasiwasi, kwamba ukishakiri basi kesho ndiyo ushahidi, siwezi kufanya kazi ya kitoto namna hiyo. Ukishasema nimetoa ‘amnesty’, msamaha maana yake ni msamaha kweli. Kwa hiyo wasiwadanganye.”

“Hao wanaowadanganya wanataka waendelee kukaa gerezani na kadiri watakavyoendelea kukaa wasije kumlaumu mtu yoyote,” amesema

Akizungumzia ombi la DPP, Mganga la kuongeza siku tatu, Rais Magufuli ameongeza siku saba kuanzia leo hadi Oktoba 6, 2019 ili watuhumiwa zaidi wajitokeze na wale ambao barua zao zilikwama kwenye ofisi za DPP na Magerezani pia wajitokeze.

“Nilitoa siku sita nikisema watuhumiwa wanaotaka kuomba kupata huo msamaha kupitia ‘process’ (njia) za kisheria na wameitikia watu 467 na fedha Sh107.842 bilioni zitatolewa na nina uhakika hawatarudia makosa yao, mimi naona niwaongezee siku saba,” amesema Rais Magufuli.

Ameongeza, “Lakini baada ya siku hizi, wale wote watakaoshikwa baada ya siku hizi nilizoongeza na wale ambao ni kesi mpya, kwa sababu kuna kesi leo mtu anaweza kuhujumu, apelekwe tu kwenye kesi za uhujumu uchumi hahusiki na huu msamaha.”