Rais Magufuli ayanyooshea kidole mashirika, kampuni 187, ayapa siku 60

Muktasari:

Wenyeviti na watendaji wakuu wa mashirika ya umma ambao hawajatoa gawio leo, wamepewa siku 60 kutoa gawio serikalini, vinginevyo waondoke wenyewe kwenye mashirika hayo ili wawapishe watu wengine kufanya kazi.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka viongozi wa mashirika, taasisi na kampuni za umma 187 kutoa gawio kwa Serikali ndani ya siku 60 na wakishindwa kufanya hivyo waondoke wenyewe kwenye nafasi zao.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumapili Novemba 24, 2019 Ikulu jijini Dodoma wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwenye taasisi, mashirika na kampuni ambazo serikali inamiliki au ina hisa zake.

Amesema Serikali ya Tanzania imewekeza mtaji wa Sh56 trilioni katika taasisi na mashirika 266, hata hivyo ameshangaa kuona ni mashirika 79 pekee ndiyo yametoa gawio kwa mwaka 2018/19 huku mashirika 187 yakishindwa kufanya hivyo.

“Baada ya siku 60, bodi za mashirika hayo 187 ambazo zitakuwa hazijaleta gawio zijivunje zenyewe, waandike barua na kama ni wa kuteuliwa na mimi maana yake siku hiyo siyo mwenyekiti tena, kama wameteuliwa na mamlaka nyingine wazivunje hizo bodi,” amesema Rais Magufuli.

Amesema haiwezekani kila mwaka shirika linajiendesha kwa hasara wakati lina mwenyekiti wa bodi na watendaji wakuu wa mashirika hayo ambao wanalipwa mishahara mikubwa.

Amesema miezi miwili ikifika hataki kuona kiongozi yoyote ambaye hajapeleka gawio anabaki kwenye shirika.

“Hatuwezi kuendelea kukaa na mashirika ya namna hii, hatuwezi kuendelea kukaa na viongozi wa namna hii, hatuwezi kuendelea kukaa na bodi za namna hii, ambazo tunazungumza lakini hawataki kuelewa,” amesema Rais Magufuli.

Amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwaandikia barua viongozi wa mashirika na taasisi hizo ambazo hazijatoa gawio na kusimamia agizo lake la kuhakikisha kwamba asiyetoa gawio aondoke.

Rais Magufuli ameyapongeza mashirika 79 ambayo yametoa gawio la Sh1.05 trilioni, ameyataka kuendelea kufanya hivyo kwa sababu serikali inatumia fedha hizo kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.

Amempongeza pia Msajili wa Hazina, Athuman Mbutuka kwa kusimamia mashirika ya umma na kuhakiki mali za umma ambazo zilikuwa zimepotelea mikononi mwa watu.

“Nafuu tuwe na mashirika machache ambayo yana-perform (yanafanya kazi vizuri) kuliko kuwa na mashirika mengi ambayo they do nothing (hayafanyi kitu),” amesema Rais Magufuli.