Rais Magufuli azungumzia fedha za ujenzi wa daraja, fidia kwa wananchi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi jijini Mwanza lenye upana wa mita 28.4  na urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.65 litakalogharimu Sh700bilioni. Ujenzi wake utadumu kwa kipindi cha miezi 48.

Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka wakazi wa Wilaya za Misungwi, Sengerema na mkoa wa Mwanza nchini humo kwa ujumla kuchangamkia fursa za ajira, uwekezaji na biashara wakati wa ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi.

Akihutubia wananchi leo Jumamosi Desemba 7, 2019 wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo refu kuliko zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Rais Magufuli ametaja makundi yanayotakiwa kuchangamkia fursa hiyo kuwa ni pamoja na wauza nafaka, vyakula, wasafirishaji na huduma zingine za kijamii.

“Mkuu wa mkoa na wote mtakaohusika katika utekelezaji wa mradi huu hakikisheni wananchi wa maeneo jirani na Watanzania kwa ujumla wanapata kipaumbele katika fursa za ajira,” ameagiza Rais Magufuli

Daraja hilo linalounganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema za mkoa wa Mwanza nchini Tanzania pamoja na mikoa ya Mwanza na Geita litakuwa ndilo daraja la sita kwa urefu barani Afrika na ujenzi wake utagharimu Sh700 bilioni.

Utakapokamilika, daraja hilo ambalo pia linaunganisha barabara zinazoenda nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) litakuwa na urefu wa Kilomita 3.2 likipita juu ya Ziwa Victoria.

Mradi huo pia utahusisha ujenzi wa barabara unganishi wenye urefu wa Kilomita 1.6. na fedha zote za utekelezaji zinatokana na mapato ya ndani.

Daraja la Kigongo-Busisi ni la sita kwa urefu barani Afrika kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu waTanroads, Patrick Mfugale ikitanguliwa na daraja lililoko nchini Misri lenye urefu wa kilomita 20.5, ikifuatiwa na lililoko nchini Nigeria lenye urefu wa kilomita 11.

Daraja la tatu kwa urefu ni Suecanal lenye kilomita 3.9 na zingine mbili ziko nchini Msumbiji zikiwa na urefu wa kilomita 3.8 na 3.6.

Akizungumzia uamuzi wa kutekeleza mradi huo kwa fedha za ndani, Rais Magufuli  amesema huo ni ushahidi kuwa Tanzania na mataifa mengine ya Kiafrika yana uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea mikopo na misaada kutoka nchi zilizoendelea.

"Sh696.2 bilioni, karibia Sh700 bilioni zinazotekeleza mradi huu siyo fedha ndogo; tena ni fedha zetu wenyewe za ndani. Hakuna mkopo na wala hatukumpigia mtu magoti kwa ajili ya fedha za kujenga daraja hili," amesema Magufuli

Amesema mbali na kupunguza adha ya kusubiri vivuko kwa muda mrefu, kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo pia utaongeza na kurahisisha shughuli za kiuchumi kati ya mikoa ya Mwanza, Geita, Kigoma na Kagera pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi na DRC.

“Pia tutaokoa maisha ya watu zilizokuwa zikipotea wakati wagonjwa wakisubiri vivuko,” amesema Rais Magufuli

Sh3.1 bilioni kufidia wananchi

Kuhusu wananchi ambao mradi wa barabara unganishi zinapitia maeneo yao, Rais Magufuli amewatoa hofu akiahidi kuwa wote watalipwa fidia.

“Fedha za kulipa fidia tayari zipo; zimetengwa zaidi ya Sh3.1 bilioni,” amesema