Rais Magufuli azungumzia shahada aliyotunukiwa Udom

Muktasari:

Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) nchini Tanzania kimemtunuku shahada ya heshima ya falsafa Rais wa nchi hiyo, John Magufuli.


Dodoma. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametunikiwa shahada ya heshima  ya udaktari wa falsafa leo Alhamisi Novemba 21, 2019 na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) akibainisha kuwa alipoelezwa kuhusu suala hilo alijiuliza sababu za kupewa bure bila kuisotea.

Rais Magufuli ametunukiwa shahada hiyo leo na Mkuu wa chuo hicho, Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

"Nilipopata barua nilijiuliza maswali mengi, kwa nini mimi?  Kwa nini sasa? Kwanini bure bila kusota...Ni ya heshima (shahada) unapewa tu na wewe unashangilia," amesema Rais Magufuli.

Amesema yeye hajawahi kupenda vitu vya dezo na hata malezi aliyolelewa nyumbani hayakuwa ya kupewa vitu bure.

Amesema  baba yake alikuwa hampi kirahisi vitu alivyokuwa akiomba na kutoa mfano kuwa akiomba kalamu alimpa kazi ya kufanya kabla ya kumpatia.

Rais Magufuli amesema wahitimu wote 6,488 hakuna alipewa bure bali wote walisotea na kwamba bure haina heshima, ni kunyimwa kujidai na inatesa.

Amesema ilimchukua mwezi mmoja kabla ya kujibu barua hiyo kwa sababu alijua hataombwa chochote kutokana na watangulizi wake kuyafanya mambo mbalimbali.

Amesema kitu kingine kilichoshindwa kujibu ni kwa sababu alikumbuka shahada hiyo si ya mtu binafsi bali ni ya Watanzania wote.