Rais Magufuli azungumzia uanzishwaji bustani za wanyama Tanzania

Muktasari:

Ili kukuza fursa za ajira na kuongeza idadi ya watalii, Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka Watanzania kuchangamkia fursa ya kufuga wanyama pori kwa sababu sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 inaeleza kuwa Watanzania wanayo haki ya kuwapata wanyamapori.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kufuga wanyamapori kupitia bustani za wanyama (Zoo).

Amesema kufanya hivyo kutachangia kuongeza idadi ya wanyama hao na kupanua fursa za utalii na ajira. 

Rais Magufuli ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na maofisa na askari wanyamapori wa Hifadhi za Taifa (Tanapa) waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita.

Amesema ufugaji wa wanyamapori unaruhusiwa kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na kwamba Watanzania wanayo haki ya kuwapata wanyamapori hao kwa mujibu wa sheria na taratibu, kuwafuga mahali popote panapofaa na patakapowezesha watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea.

Amesema kuna nchi nyingi ambazo wananufaika kwa ufugaji wa wanyamapori ikiwamo Afrika Kusini, wanapata watalii wengi, watu wanapata ajira na wanaowekeza kwenye ufugaji huu wanapata fedha.

“Nawapongeza baadhi ya Watanzania walioanzisha Zoo hizo wakiwamo Luteni Jenerali mstaafu Samwel Ndomba (Lugari Mini Zoo – Mbinga), Dar es Salaam Zoo, Bahari Zoo na wengine ambao wamefuga wanyamapori katika bustani na mashamba yao.”

“Nawaomba na wengine changamkieni fursa hii ndugu zangu, wataalamu wa wanyamapori wafundisheni wananchi kufuga wanyamapori na wahamasisheni kufanya hivyo,” amesema Rais Magufuli

“Viongozi wastaafu jitokezeni kuonyesha mfano kama alivyofanya Ndomba kule Mbinga, maeneo ya kufuga yapo mengi.”