Rais Mstaafu Kikwete ashangaa walimu kukosa ajira

Raisi Mstaafu Jakaya Kikwete (katikati) akiwa kwenye mandamano jana kuelekea Viwanja vya Chuo Kikuu huria cha Tanzania  muda mfupi kabla ya kwanza kwa sherehe za  mahafari ya 37 ya Chuo hicho yaliyofanyika jana Kibaha Mkoani Pwani wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarit Ndikilo na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda. Picha na Sanjito Msafiri

Kibaha. Wakati wimbi la wahitimu likiendelea kuongezeka nchini, Rais mstaafu Jakaya Kikwete ameeleza kusikitishwa na idadi kubwa ya walimu kuwepo mitaani kwa kukosa ajira licha ya upungufu wao kwenye shule nchini.

Kikwete ametoa kauli hiyo jana ikiwa zimepita siku 14 tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipolieleza Bunge mkakati wa Serikali wa kuajiri walimu 16,000 wa shule za msingi na sekondari.

Majaliwa alisema hayo Novemba 14, wakati akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi ambaye alihoji mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wanapatikana watumishi wa kutosha kuwahudumia wananchi.

Hata hivyo, Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 37 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika makao makuu ya chuo hicho Bungo, Kibaha mkoani Pwani alizungumzia mpango aliouanzisha wa kuzalisha walimu wakati wa uongozi wake.

Alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuboresha elimu nchini kwa nyakati tofauti huku akigusia utaratibu aliouanzisha kwenye utawala wake uliokuwa unawaruhusu wahitimu wa kidato cha sita kwenda kuchukua mafunzo ya ualimu mpango ambao baadaye ulisitishwa.

Kikwete alisema wakati anamaliza kipindi chake cha urais aliacha idadi kubwa ya walimu nchini na baada ya hapo wameendelea kuwa wengi kiasi ambacho wapo wanaokosa nafasi za ajira.

“Tulianzisha mpango uliokuwa unawawezesha wahitimu wa kidato cha sita kwenda kuchukua mafunzo ya ualimu nia ikiwa ni kuzalisha walimu wengi mpango uliokuwa unaitwa vodafasta,” alisema Kikwete aliyekuwa Rais kati ya mwaka 2005 hadi 2015.

Alisema jitihada zingine kwenye uongozi wake katika kuboresha elimu ilikuwa ni pamoja na ujenzi wa shule za sekondari za kata, ambapo walikumbana na changamoto ya uhaba wa walimu wakaja na mpango huo wa mafunzo ya vodafasta.

Akizungumzia kauli hiyo ya Kikwete, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo aliiambia Mwananchi jana kuwa mpango huo ulisitishwa kutokana na kukosa tija kutokana na kuwepo walimu wa kutosha.

Dk Akwilapo alisema mpango huo haukuwa na tofauti na ule wa `Elimu kwa Wote’ (UPE) mwaka 1974/75 ulitumika kuongeza walimu.

Kuhusu ukosefu wa ajira za walimu, Katibu mkuu huyo alisema suala hilo liko chini ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Naye Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara alipoulizwa kuhusu suala hilo la ajira kwa walimu alijibu, Serikali inakusudia kuajiri walimu 16,000.

“Hili alilisema Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) bungeni wakati akijibu swali la Mbunge (wa Mlalo- CCM, Rashid) Shangazi,” alifafanua Waitara.

Waitara alieleza serikali chini ya Rais mstaafu Kikwete ilianzisha mpango wa kuandaa walimu wa haraka kwa sababu wakati huo kulikuwa na upungufu.

“Kwa sasa tuna walimu wa kutosha wenye ubora wa kufundisha vyuo, sekondari, shule za msingi na awali, changamoto ni uwezo wa Serikali kuajiri walimu wa kutosha na Serikali itakuwa ikiajiri kulingana na uwezo wa fedha,” alisema Waitara

Pia katika mahafali hayo ya OUT, Kikwete alitahadharisha kutokana na tekInolojia inavyoendelea kwa kasi duniani, hali inaonyesha ifikapo mwaka 2050 nusu ya kazi zinazofanywa na binadamu kwa sasa zitakuwa zinafanywa na mashine.

Alisema kulingana na hali hiyo pia nafasi hizo zitakuwa zinawalenga wahitimu wa elimu ya juu huku wa elimu ya kawaida wakishindwa kupata nafasi.

Jumla ya wahitimu 3,900 wa shahada mbalimbali walitunukiwa na Mkuu wa Chuo hicho, Mizengo Pinda ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu.

Mmoja wa wahitimu kwenye mahafali hayo alikuwa ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa aliyetunukiwa shahada ya uzamivu (PhD), ambaye aliwataka watumishi wa umma nchini wenye lengo la kujiendeleza kufanya mawasiliano na waajiri wao kabla ya kujiunga na masomo ili kupewa maelekezo muhimu na njia za kufuata.

Alisema Serikali haina lengo la kuwazuia watumishi wake kujiendeleza kitaaluma bali inawaruhusu kufanya hivyo iwapo wanafuata utaratibu.

Dk Mary alisema aliamua kujiendeleza kielimu ili kuongeza weledi wake kwenye kutekeleza majukumu yake kwa umma.