Ripoti ya CAG yabaini NDC kushindwa kuendeleza baadhi ya maeneo

Muktasari:

Ripoti ya CAG imebaini namna Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lilivyoshindwa kuendeleza asilimia 77 ya maeneo maalum yaliyokuwa yametengwa wa ajili ya viwanda

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imesema Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeshindwa kuendeleza hekta 250.42 sawa na asilimia 77 ya maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda.
Maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya viwanda ni hekta 74.11 za eneo la TAMCO-Kibaha, hekta 229 za eneo la KMTC Moshi na hekta 23 za eneo la Kange mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo maeneo ambayo hayajaendelezwa ni hekta 14.42 za TAMKO, hekta  213 za KMTC na hekta 23 za Kange.
“Katika mapitio ya mpango mkakati wa maendeleo wa Shirika la Taifa la Maendeleo wa mwaka 2018/2019 - 2022/2023, nilibaini utekelezaji duni wa mpango wa shughuli za mwaka katika kuendeleza maeneo maalumu ya viwanda,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo ya CAG.
Ripoti hiyo imesema NDC ilishindwa kujenga mabwawa ya maji taka, matenki ya kuhifadhi maji safi na vituo vidogo vya kupokea umeme ndani ya eneo la TAMCO.
“Nilibaini kwamba wawekezaji katika eneo la viwanda TAMCO wanajenga miundombinu yao wenyewe kama vile kujenga mabwawa ya majitaka, kujenga matanki ya kuhifadhia maji safi, kujenga pamoja na vituo vidogo vya kupokea umeme,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza;
“Hali hii inaweza kusababisha kutengeneza miundombinu inayotofautiana ya chini ya kiwango, au isiyofaa kwani kila mtu anafanya kwa matakwa yake bila kufuata mwongozo.
Kukosekana kwa miundombinu muhimu kunaleta changamoto kubwa katika kuvutia uwekezaji, hali hii inasababisha shirika kushindwa kufikia malengo yake.”
Kutokana na hali hiyo ripoti hiyo ya CAG 2020 ilipendekeza NDC ihakikishe inatekeleza mipango yake kwa wakati kama ilivyoainishwa katika mpango mkakati wake wa maendeleo.
“Vilevile, libuni mpango mkakati ambao utaisaidia maendeleo ya sehemu zote ambazo bado hazijaendelezwa ndani ya maeneo yaliyotengwa maalumu kwa ajili ya viwanda,” imeandika sehemu ya ripoti hiyo.