Ripoti ya CAG yabaini madudu katika taasisi za umma

Dodoma. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeendelea kubaini dosari ya matumizi za fedha yanayofanywa na taasisi na mashirika ya umma pamoja na vyama vya siasa.

Mbali na kasoro za ukaguzi, pia taasisi 41 kati ya 189 alizozikagua hazikupata hati yoyote kwa sababu mbalimbali ikiwamo kuchelewesha majibu ya hoja za ukaguzi.

Kichere alikuwa ameongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka na makamu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota, wakati akitoa ripoti ya ukaguzi wake kwa waandishi wa habari Dodoma jana.

Ukaguzi alioufanya kwa taasisi za Serikali Kuu, mamlaka ya serikali za mitaa, mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na vyama vya siasa ni wa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2019.

Kichere pia alizungumzia kuongezeka kwa deni la Serikali kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kwamba alibaini kuwa deni la Serikali limeongezeka kwa Sh16.18 bilioni kutoka Sh37.45 bilioni za mwaka uliopita.

“Nina mashaka kuwa ukwasi wa Bohari unazidi kushuka, hivyo kuathiri utekelezaji wa mipango mbalimbali ikiwamo usambazaji wa dawa na vifaa tiba kwa jamii pamoja na utekelezaji wa mipango yake mbalimbali.

Kuhusu TTCL, alisema alibaini kuwa shirika hilo lililoingia mkataba na Kampuni ya MIC Tanzania kwa ajili ya kupitisha mawasiliano (roaming) yake ya kitaifa imepata hasara ya Sh1.11 bilioni.

Alisema TTCL imekuwa ikitoza vifurushi kwa bei rahisi tofauti na wanavyonunua MIC.

“Mfano, GB 1 TTCL wanauza kwa Sh1,500, lakini wao wanainunua MIC kwa Sh2,500, hivyo kusababisha hasara ya Sh1,000 kwa kila GB.

Kichere alisema amebaini deni la Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii na Bima ya Afya ni Sh2.42 trilioni.

Alisema mifuko yote ya hifadhi ya jamii na Bima ya Afya ina madai makubwa ambayo ni kichefuchefu, mengi ya madeni hayo ni kwa Serikali na taasisi zake.

“Mpaka kufikia Juni 30, 2019, mifuko hiyo ilikuwa inaidai Serikali pamoja na taasisi zake kiasi cha Sh2.42 trilioni. NSSF wanadai Sh1.47 trilioni, PSSF Sh731.40 bilioni na NHIF Sh220.39 bilioni,” alieleza Kichere.

Kichere alisema ukaguzi wake ulibaini madai yaliyokosa uthibitisho ya jumla ya Sh291.17 bilioni.

“Wakati wa uhakiki wa madeni ya Shirika la Uzalishaji Umeme Tanzania (Tanesco) niliomba uthibitisho wa madeni ya kutoka kwa wadeni ambapo ni kampuni 23 pekee ndizo zilizoweza kuthibitisha madeni yao yenye thamani ya Sh647.33 bilioni.

“Huku kampuni 913 zenye madai yenye thamani ya Sh291.17 bilioni hazikuweza kuthibitisha madai yao, kati yao ipo kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) yenye jumla ya madai ya Sh102.12 bilioni,” alisema.

Kicheere alisema katika ukaguzi wake alitoa jumla ya hati 1,082 za ukaguzi. Hati zinazoridhisha ni 1,017, hati zenye shaka ni 46, hati zisizoridhisha ni saba na hati mbaya ni 12.

Kati mashirika 189 aliyoyakagua 148 ndiyo yalipata hati huku 41 yakiwamo Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), Makumbusho ya Taifa Tanzania, Stamico, Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Magazeti Tanzania (TSN), Shirika la Simu Tanzania (TTCL) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Veta), hayakupata hati.

Kichere alisema pia alibaini taasisi tano za Serikali Kuu zilifanya manunuzi ya vifaa na huduma yenye thamani ya Sh5.46 bilioni pasipokuwa na mikataba.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walinunua sare la jeshi kutoka kwa mzabuni 21 Century Textiles Ltd (Sh4,242,319,008), Wizara ya mambo ya Ndani ununuzi wa nyaya za LAN (Sh 28,667,583).

Alisema amebaini dosari ya Sh806.69 milioni kwenye malipo yaliyofanywa na Jeshi la Polisi katika ujenzi wa nyumba 400, mabweni na vyumba vya madarasa.

Kichere alizitaja baadhi ya dosari hizo ni malipo kwa vibarua kabla ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi (Sh355.2 milioni) na malipo ya kwenye akaunti binafsi badala ya fundi mchundo aliyesaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa jengo la makao makuu ya polisi Dodoma (Sh145.2 milioni).

Kichere alieleza kubaini mapungufu kwenye balozi za Tanzania nje ya nchi ni matumizi yasiyo na tija ya Sh1.02 bilioni kwa ajili ya kulipia makazi, wakati nyumba zinazomilikiwa na Serikali zipo, isipokuwa zinahitaji ukarabati.

“Nimebaini kuwa balozi za Tanzania nchini Brazil, Algeria na Sweden zilizotumia Sh1.02 bilioni kukodi nyumba za makazi, kiasi ambacho kingeweza kuepukika kwa kukarabati nyumba za makazi zilizochakaa,” alisema.

Alisema ubalozi wa Tanzania nchini Brazil ulitumia Sh274,061,808, Algeria ulitumia Sh514,095,600 na Sweden ulitumia Sh228,045,300.

Pia, alisema balozi tano zilifanya malipo yanayofikia Sh645.07 milioni, ambayo hayakuwa na nyaraka toshelezi.

Kichere alisema alibaini balozi 14 zina majengo yaliyotelekezwa kwa muda mrefu yanayohitaji ukarabati mkubwa ili kuendelea kutumia.

Alisema alibaini balozi nane zilipewa viwanja kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi na havijaendelezwa kwa muda mrefu.

Maoni ya kamati

Mwenyekiti wa PAC, Kaboyoka alisema hoja ya kamati yake ilikuwa viporo vimalizike kabla ya Bunge, lakini mashirika ya umma na taasisi za Serikali yameendelea kucheza na fedha za umma.

Alisema kwa kutaka kuficha siri kuna baadhi ya taasisi na mashirika walidiriki kuwahamisha wakaguzi wa ndani na kuwapeleka pembezoni huku wakiajiri wapya.