VIDEO: Ripoti ya CAG yabaini mapungufu CUF, CCM

Muktasari:

  • Kichere amebainisha kwamba katika ukaguzi wake alibaini kwamba chama cha CUF kilipokea ruzuku ya Sh369.38 milioni lakini kiasi cha Sh300 milioni kilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya chama kwenda kwenye akaunti binafsi.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebainisha mapungufu katika ukaguzi wake kwenye vyama vya siasa vya CUF na CCM.
Kichere amebainisha hayo leo Alhamisi Machi 26 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati akiwasilisha ripoti ya ukaguzi wake ya 2018/19 kwa Rais John Magufuli.
Kichere amebainisha kwamba katika ukaguzi wake alibaini kwamba chama cha CUF kilipokea ruzuku ya Sh369.38 milioni lakini kiasi cha Sh300 milioni kilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya chama kwenda kwenye akaunti binafsi.
Pia, amesema chama hicho kimeondoa saini ya katibu mkuu kama mmoja wa watu wa kuidhinisha utoaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya chama.
"Ninashauri mifumo ya udhibiti wa fedha ndani ya chama iimarishwe kwa kufuata sheria na katiba ya chama," amesema Kichere wakati akiwasilisha ripoti yake ya ukaguzi.
Kwa upande wa CCM, Kichere amesema Jumuiya ya Wazazi ilimuondoa mpangaji wake bila kufuata utaratibu, jambo lililosababisha mpangaji kutishia kufungua kesi akitaka kulipwa fidia ya Sh800 milioni.
Hata hivyo, amesema jumuiya hiyo ilimlipa Sh60 milioni baada ya kufanya mazungumzo ya kirafiki na mpangaji huyo ili kumaliza mgogoro uliokuwepo.
"Jumuiya ya wazazi ifuate utaratibu na masharti yaliyopo katika mikataba yao. Hiyo itaepusha kulipa fedha ambazo zingeweza kuepukika," amesema Kichere.