Rooney atarajia Harry Kane kufikia rekodi yake ya mabao England

Saturday September 14 2019
roonpic

London, Uingereza (AFP). Wayne Rooney amesema Harry Kane anaweza kuvunja rekodi yake ya kuifungia England mabao mengi katika kipindi cha "miaka miwili au mitatu ijayo".

Rooney alifunga mabao 53 akiichezea England katika kipindi chake alichong'ara na kwa idadi hiyo mshambuliaji huyo wa zamani wa  Manchester United alivunja rekodi ya mabao 49 iliyowekwa na gwiji wa soka wa England, Bobby Charlton.

Lakini Rooney, ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya DC United ya Marekani kabla ya kuhamia Derby Count mwezi Januari, anaamini kuwa nahodha huyo wa England yuko mbioni kuvunja rekodi yake.

Mshambuliaji huyo wa Tottenham ameshafunga mabao 26 baada ya kuziona nyavu katika mechi za michuano ya kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2020 dhidi ya Bulgaria na Kosovo.

"Sikuchukulia kama mabao yangekuja,napenda kufunga mabao. Nilipofikisha mabao 35 nikiwa timu ya England, nilihisi rekodi ilikuwa inakaribia," alisema Rooney.

"Sidhani kama (rekodi yangu) itadumu kwa miaka 50 kama ya Bobby Charlton, nadhani Harry Kane, anaweza kuifikia katika miaka miwili au mitatu ijayo. Ni mfungajki mzuri na rekodi yake kwenye timu ya England ni nzuri.

Advertisement

"Wakati nilipofikia rekodi na kwenda kucheza mechi yangu ya mwisho nilisema itakuwa ni heshima kwenda na kumkabidhi kama Bobby Charlton alivyonikabidhi kiatu cha dhahabu na nina uhakika haitachukua muda mrefu."


Advertisement