Rubani mwanafunzi aliyekufa ajali ya ndege aliomba kuchangiwa ada

Muktasari:

Nelson Orutu, rubani mwanafunzi aliyefariki dunia juzi Septemba 23, 2019 katika ajali ya ndege aliomba kuchangiwa fedha na wenzake ili alipe ada kuhitimu mafunzo ya urubani katika Chuo cha Nairobi Huston Aiport.

Arusha. Nelson Orutu, rubani mwanafunzi aliyefariki dunia juzi Septemba 23, 2019 katika ajali ya ndege aliomba kuchangiwa fedha na wenzake ili alipe ada kuhitimu mafunzo ya urubani katika Chuo cha Nairobi Huston Aiport.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Septemba 25, 2019 na rubani David Mwano wakati akizungumza na Mwananchi.

Nelson Orutu na Nelson Mabeyo, mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Venance Mabeyo, walifariki dunia katika ajali ya ndege ya kampuni ya Auric Air iliyoanguka katika uwanja mdogo wa ndege wa Seronera uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Nelson Mabeyo alikuwa rubani katika ndege hiyo iliyoanguka juzi saa 1:30 asubuhi wakati ikipaa kutoka uwanja huo kwenda mkoani Arusha na Nelson Orutu alikuwa rubani mwanafunzi.

Katika maelezo yake Mwano amesema Olutu alikuwa anaipenda urubani na alijitahidi katika masomo.

"Nakumbuka aliwahi kuanzisha kundi mtandao wa kijamii la WhatsApp la marubani tuchange fedha kumuongezea ada, tulimchangia kwa sababu alikuwa anapenda sana urubani,” amesema.

Amesema Olutu amefariki akiwa akaribia kuhitimu mafunzo  katika chuo hicho, kwamba alikuwa amepata leseni ya kwanza ya kuendesha ndege na alikuwa anakamilisha apate leseni ya pili.

“Marubani wengi walikuwa wanamfahamu Orutu na walisafiri naye. Hiyo iliyokana na mapenzi yake katika urubani.

Kelvin Orutu, kaka wa Nelson Orutu amesema baadaye leo watatoa taarifa za mazishi ya mdogo wake.