Advertisement

Rugemalira ashangaa kuendelea kushtakiwa, atoa notisi kwa taasisi tisa

Thursday February 13 2020
ruge pic

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa kampuni ya VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, James Rugemalira  amewasilisha notisi kwa taasisi tisa nchini Tanzania  akitaka Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) amuondoe kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.

Ameeleza kuwa asipofanya hivyo atawasilisha rasmi hoja za kuondolewa katika kesi hiyo mahakamani.

Januari 30, 2020 mfanyabiashara huyo aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwa  ameandika barua kwenda kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akielezea jinsi gani benki ya Standard Chartered ya Hong Kong walivyokuwa wakikwepa kodi na ushuru wa forodha.

Siku hiyo alidai Januari 24, 2020 aliongea na mwakilishi wa Takukuru alipotembelea gerezani na akamkabidhi nakala ya barua hiyo aliyoandika kwenda kwa Kamishna  wa TRA lakini hadi sasa hajapata jibu lolote.

Pia, aliomba kesi hiyo ilitajwa tena, yaani leo upande wa mashtaka kuleta majibu kwa sababu wanaostahili kushtakiwa katika kesi inayomkabili ni benki hiyo.

Leo Alhamisi Februari 13, 2020 Rugemalira ametoa notisi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Advertisement

"Mheshimiwa hakimu nilitoa notisi sehemu mbalimbali ikiwemo kwa DPP na tayari imepokelewa, leo hii nilitegemea naachiwa  kwa kuondolewa katika shauri hili,” amesema Rugemalira.

Miongoni mwa taasisi alizopeleka notisi ni ofisi ya DPP, DCI (mkurugenzi wa makosa ya jina),  Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Mkurugenzi wa Takukuru, Gavana wa Benki Kuu, Kamishna TRA, wakili mkuu wa Serikali, DK Clement Mashamba na Kamishna wa Magereza.

Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili Rugemalira na mwenzake Harbinder Seth ni kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha  na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh309 bilioni

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa  kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India

Katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam wakiwa si watumishi wa umma  walitekeleza mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la tatu, Seth anadaiwa  Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam, akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa kampuni  na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi kiwanja namba 887 mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.

 

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi

Advertisement