Rugemalira awataja wezi wa Escrow

Muktasari:

Ameiomba mahakama hiyo imruhusu kwenda nje ya nchi kwaajili ya uchunguzi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kansa kwa miaka tisa

 Mfanyabiashara James Rugemalila anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi leo Ijumaa ametaja wanaohusika  na wizi wa fedha katika akaunti ya Escrow. 

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Rugemarila ameiomba mahakama hiyo imruhusu kwenda nje ya nchi kwaajili ya uchunguzi kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa kansa kwa miaka tisa.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leornad Swai kueleza kuwa bado upelelezi wa kesi hiyo unaendelea hivyo anaomba Mahakama ipange tarehe nyingine.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Michaeli Ngalo ameuomba upande wa mastaka kuharakisha upelelezi na kama umeshindwa basi waitoe kesi hiyo mahakamani.

Baada ya wakili wake kueleza hayo Rugemarila alinyoosha mkono akimweleza Hakimu kuwa anasumbuliwa na kansa kwa muda wa miaka tisa hivyo anaomba akapatiwe matibabu India kwani uvimbe umejitokeza.

"Nilikuwa sijui kama nina uvimbe sehemu za siri, huu mwaka mpya umenijia vibaya, naomba nipewe ruhusa kwenda India kwa daktari wangu ili nikafanyiwe uchunguzi,"

Rugemarila alidai alishawasilisha nyaraka za ushahidi Takukuru zikionyesha nani mwizi aliyeisababishia Serikali hasara.

"Mwizi ni Benki ya Standard Chartered iliyoko hapa nchini Tanzania Ltd na ile  iliyoko Hong Kong ambazo ndio zimesababisha hasara ya Trillion 37 kwa Serikali,”

"Pia kuna nyaraka nilizozipelekaTakukuru zikionyesha wengine walioshiriki katika wizi wa fedha hizo, naomba niendelee kuwa hai ili niweze kutoa ushahidi mzuri kuhusu wezi wa fedha hizo.”

Mshtakiwa mwingine ambaye ni mmiliki wa IPTL Harbinder Singh Sethi ameieleza Mahakama kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano ikiwemo nyaraka zitakazoitajika.

Hata hivyo, wakili Swai alieleza Mahakama kuwa zipo nyaraka ambazo Rugemarila aliwasilisha  ofisini na zinafanyiwa kazi kisha watatoa majibu baada ya kukamilika.

Hakimu Simba alisema afya za washtakiwa ni muhimu wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi na kuutaka upande wa mashtaka ukamilishe upelelezi kwa wakati.

Kesi hiyo imeairishwa hadi Januari 19, 2018 itakapotajwa tena.