Rugemarila, Seth kula Krismasi gerezani

Muktasari:

Juni 19 mwaka 2017, washtakiwa James Rugemarila na Herbinder Seth walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wakikabiliwa na mashtaka 12 ikiwamo ya uhujumu uchumi ambapo mpaka sasa upelelezi wa mashtaka hayo haujakamilika.

Dar es Salaam. Washtakiwa James Rugemarila na Herbinder Seth wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi watakula sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya 2020 kwa mara ya tatu wakiwa gerezani.

Washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Juni 19 mwaka 2017 wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwamo ya uhujumu uchumi, kula njama na kujihusisha na mtandao wa uhalifu.

Leo Alhamisi Desemba 19, 2019 Wakili wa Serikali ya Tanzania, Ester Martin ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mmbando kuwa kesi hiyo imekuja kwaajili ya kutajwa, upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwaajili ya kutajwa.

"Kesi imekuja kwaajili ya kutajwa, upelelezi wa shauri hili bado haijakamilika tunaomba tarehe nyingine kwaajili ya kutajwa na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia," amedai Ester

Mawakili wa upande wa utetezi, Pascal Kamala na Dorah Malaba wamedai hawana pingamizi na maelezo ya wakili wa serikali.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 2, 2020 kwaajili ya kutajwa.

Katika kesi ya msingi, Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh309.46 bilioni

Washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba 18 mwaka 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Aidha, inadaiwa katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh309. 46 bilioni. 

Pia, washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh309.46 bilioni.