Breaking News

Rwanda ya pili Afrika Mashariki kuhalalisha kilimo cha bangi

Friday October 16 2020

 

By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Rwanda imehalalisha kisheria kulima bangi na kuiuza nje kwa ajili ya matumizi ya tiba na nchi kujipatia fedha.

Licha ya ruhusa hiyo, bado sheria ya nchi hiyo zinazuia kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi mengine kama uvutaji.

Rwanda inakuwa nchi ya pili ya Afrika Mashariki kuruhusu uzalishaji wa bangi kwa ajili ya mauzo ya nje, baada ya Uganda kutangaza kuuza bangi yake katika masoko ya Ulaya Agosti mwaka jana.

Hatua hiyo ya Uganda ilikuja baada ya wakaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuidhinisha nchi hiyo kuingiza bangi Ulaya.

Taarifa iliyopatikana jana katika tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ilieleza kuwa kikao cha baraza la mawaziri Uganda kilichokaa Oktoba 12 kiliidhinisha miongozo ya kilimo, usindikaji na mauzo ya nje ya mimea ya matibabu ya thamani ya juu nchini Rwanda.

Akizungumza na televisheni ya taifa hilo jana Waziri wa Afya wa Rwanda, Dk Daniel Ngamije alisema mimea iliyoruhusiwa kulimwa kwa ajili ya dawa inajumuisha bangi.

Advertisement

Taifa hilo lililopo Afrika mashariki limehalalisha bangi baada ya nchi kama Malawi, Lesotho, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe kuhalalisha kisheria mauzo ya bangi na matumizi ya mmea huo.

Ngamije alisema Rwanda inataka kutoa mchango wake katika utafiti wa dawa ili kujipatia fedha.

“Rwanda inataka kutoa mchango wake kwa vituo vya utafiti na sekta ya dawa kwa kutoa raslimali ili tupate faida ya fedha…”

Mwaka jana, soko la bangi la dunia lilikadiriwa kuwa na thamani ya dola 150 billion, kwa mujibu wa Benki ya Barclays.

Bodi ya Maendeleo ya Rwanda imesema ni wakulima waliopewa leseni pekee ndio watakaoruhusiwa kuzalisha zao hilo.

“Uvutaji wa bangi bado unazuiwa,” imeongeza taarifa ya bodi hiyo.

Kwa mujibu wa sheria za Rwanda ukipatikana unalima au kuuza bangi unaweza kufungwa hadi kifungo cha maisha jela, huku mvutaji akikabiliwa na kifungo cha miaka miwili jela nchini Rwanda.

Gazeti la The Daily Monitor la Uganda linaeleza kuwepo kampuni 50 zilizoomba kibali Wizara ya Afya ya nchi hiyo kuungana na kampuni ya Industrial Globus Uganda Ltd kuzalisha bangi kwa ajili ya matibabu.

Wakati hali ikiwa hivyo Rwanda na Uganda, baadhi ya wabunge haoa nchini wamekuwa wanasukuma ajenda bungeni ya kutaka kuhalalishwa kwa zao hilo.

Februari mwaka huu, Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba aliibua hoja hiyo bungeni akiomba Serikali kuhalalisha kilimo cha bangi wakati akichangia taarifa ya kamati ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Kishimba aliitaka Serikali kuhalalisha kilimo cha bangi kwa lengo la kutengeneza dawa za mifugo na binadamu ambavyo imeruhusiwa katika baadhi ya nchi za Afrika.

Mbali na Kishimba, Mbunge wa Geita Mjini, Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma alisisitiza hoja hiyo akishauri kuundwa kwa kanuni za kurasimisha kilimo cha bangi.

Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji), Angela Kairuki alisema tayari kuna mchakato mezani kwake wa uwekezaji wa mafuta ya bangi ambao wizara yake inaendelea kuuchanganua kabla ya kutoa taarifa yake.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, uratiobu wa Bunge, kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu), Jenista Mhagama alisema kwa sasa hakuna sheria wala kanuni zinazoruhusu kilimo, usindikaji wa matumizi ya bangi.

Advertisement