SIASA: Mambo matano kutikisa Bunge

Dodoma. Mkutano wa 18 wa Bunge la 11 unaanza kesho, ukitarajiwa kuwa na mambo kadhaa yatakayoibua mijadala ndani na nje, ikiwamo kurejea kwa mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye ameahidi kutobadilika baada ya kumaliza adhabu ya kuzuiwa kuhudhuria mikutano ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Kabla ya Bunge kuanza kesho, kulikuwa na vikao vya kamati mbalimbali kwa ajili ya mkutano huo wa 18.

Baada ya vikao hivyo vya wiki mbili, Bunge la 11 litakuwa limebakiwa na mkutano mmoja, ambao ni wa Bunge refu la Bajeti ma baaadaye litavunjwa na Rais John Magufuli ili kupisha uchaguzi mkuu.

Lema kurudi mjengoni

Moja ya matukio yatakayopokelewa kwa mitazamo tofauti ni la kurejea kwa Lema, ambaye alipewa moja ya adhabu kubwa na Bunge hilo baada ya kufungiwa kushiriki mikutano mitatu kuanzia Aprili 4, mwaka jana, kipindi ambacho ni takriban mwaka mzima. Alipatikana na kosa la kulidharau na kulidhalilisha Bunge.

Anaweza kupokelewa kwa shangwe na wabunge wa upinzani, kitu ambacho hakitakubaliwa na wabunge wa CCM.

Adhabu iliyomtia kifungoni mbunge huyo ni kuunga mkono kauli ya aliyekuwa Mkaguzi na Msimamizi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad aliyesema mhimili huo wa nchi “ni dhaifu” alipoulizwa na redio ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kutofanyiwa kazi kwa mapendekezo ya ripoti za ukaguzi.

“Hatujawahi kuwa na mapambano madogo au hafifu,” alisema Lema alipoulizwa kama atabadilisha utendaji wake baada ya adhabu hiyo.

“Sisi tuko imara na kipindi hiki morali ni ule ule wa kuisimamia Serikali. Wana-Arusha wanaelewa sana na wanafahamu wajibu wangu. Nilipokuwa nje ya Bunge walielewa na hawatarajii mimi kuwa nyuma.”

Lema, ambaye ni waziri kivuli wa Mambo ya Ndani, ataingia bungeni wakati sakata la kuondolewa uwaziri kwa Kangi Lugola likiwa halijapoa. Lugola alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na ameondolewa kutokana na wizara yake kusaini mkataba mbovu ambao ulikiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma na hakupata baraka za Bunge.

Lugola kurudi benchi

Kama ilivyo kwa wabunge kadhaa ambao huteuliwa kuwa mawaziri na baadaye uteuzi wao kutenguliwa, mkutano unaoanza kesho pia utashuhudia Lugola akirejea katika viti vya kawaida ndani ya ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria. Alivuliwa uwaziri hadharani kutokana na mkataba uliotayarishwa na wizara hiyo wenye thamani ya zaidi ya Sh1 trilioni unaohusu ununuzi wa vifaa vya uokoaji lakini ukasainiwa bila kufuata taratibu.

Rais Magufuli alisema mradi uliomponza Lugola ulitayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto, Thobias Andengenye ambao haujapangwa kwenye bajeti wala kupitishwa na Bunge.

Nafasi ya Lugola imechukuliwa na mbunge wa Kibakwe (CCM), George Simbachawene ambaye anakabiliwa na kibarua cha kusafisha madudu katika wizara hiyo.

Uchaguzi mkuu

Pia, Bunge linarejea kazini huku kukiwa na hoja kuhusu kauli ya Rais Magufuli aliyoitoa kwenye hafla ya mabalozi ya kuukaribisha mwaka mpya (Sherry party) iliyofanyika wiki iliyopita Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu unakuwa wa amani, uhuru na wa haki.

Ahadi hiyo ya Rais Magufuli imeibua mjadala miongoni mwa wanasiasa na wasomi, baadhi wakiunga mkono na wengine wakihoji uthabiti wa utekelezaji wake.

Ni kawaida wabunge wa upinzani kuchomokea hoja kama hizo kila wanapochangia shauri vikaoni na kupingwa na mawaziri husika au wabunge kutoka chama tawala.

Hoja ya wapinzani ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi na kuruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kuufanya uchaguzi uwe huru na wa haki, wakati Serikali hutetea kuwa tume iliyopo ni huru.

Mkakati wa kutumia mahakama kuwaondoa wakurugenzi wa wilaya kusimamia uchaguzi ulikwama baada ya Serikali kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

“Tutatumia nafasi hii kuwasha moto wa kudai tume huru ya uchaguzi, kama ambavyo chama chetu kimesisitiza,” alisema mbunge wa Mlimba, Susan Kiwanga.

Kiwanga alisema mkutano huu watautumia kudai mabadiliko ya tume kwa kuwa Tanzania inaingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani na kila chama kinataka kushika dola.

Suala la mikataba ya madini

Pia, mkutano huu wa Bunge unatarajiwa kuibua hoja ya tukio la utiaji saini mikataba tisa kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold, lililofanyika wiki iliyopita.

Makubaliano hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam ni matunda ya mazungumzo kati ya Serikali na kampuni hiyo tangu mwaka 2017 yaliyozaa kampuni ya Twiga itakayosimamia migodi mitatu iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

Baadhi ya wabunge wanasema mkataba na Barrick umekiuka sheria zilizopitishwa na Bunge kuhusu usuluhishi endapo kutatokea ukiukwaji wa mkataba na suala la dola 300 milioni za Kimarekani zilizoahidiwa na Barrick kama kishika uchumba lakini hazijawekwa bayana wakati wa kusaini mikataba hiyo.

Mzozo huo ulitokana na usafirishaji nje wa makinikia kwa ajili ya kwenda kuyeyushwa kupata mabaki ya madini yaliyoshindikana kutolewa wakati wa uchenjuaji migodini enzi ya kampuni ya Acacia, iliyokuwa inasimamia migodi ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu.

Sakata hilo lilisababisha Rais aunde kamati iliyochunguza na kuibua kasoro kadhaa zilizoondoa mawaziri na watumishi wa umma.

Bunge la lala salama

Mkutano unaoanza leo pia unatarajiwa kuendeleza siasa za uchaguzi wa ubunge zilizoanza katika kikao kilichopita.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema litakuwa Bunge la aina yake kwa kuwa ni la “lala salama”.

Lusinde, maarufu kama Kibajaji, alisema jana kuwa Bunge hili litafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, lakini wananchi wanakwenda kuchuja kati ya pumba na mchele na hilo litafanyika kwa kuangalia hoja.

“Serikali imefanya mambo makubwa na Rais ametimiza ahadi zake, hasa za kutumbua kwa hiyo wananchi wategemee tunakwenda kumaliza kazi kwa kishindo,” alisema Kibajaji.

Naye Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali alisema ni Bunge la lala salama na kuwa wabunge wa kweli na wabunge wa maslahi watajulikana.

Maoni kama hayo pia yalitolewa na Lema. “Umebaki muda mfupi sana kabla ya Bunge kuvunjwa. Ni Bunge fupi lakini kila mbunge anafikiria zaidi kutetea kiti hasa wale wanaotarajia kugombea tena,” alisema.

“Wabunge watataka kuonyesha uwezo wao.”