SIMULIZI ZA MZIKI: Madansa jana na leo

Karibu kila bendi kubwa siku hizi huwa inakuwa na kundi la wasanii ambao kazi yao ni kucheza dansi. Jina maarufu la wasanii hawa lilikuwa ni ‘Stage Show’. Siku hizi huitwa Wacheza Show au Madansa. Mara ya kwanza mimi kuwaona wacheza shoo jukwaani ilikuwa mwaka 1962 wakati Dorothy Masuka na kundi lake lilipopita Iringa na kufanya onyesho katika ukumbi wa Highland Cinema, nilikuwa mdogo sana lakini kilichobakia kichwani ni kumbukumbu ya wachezaji wake waliovaa vibwaya na Dorothy Masuka akiimba wimbo wa Patapata.

Hivyo swala la kucheza shoo si jambo jipya japo limepitia katika mabadiliko mbalimbali. Miaka ya 1960, wacheza shoo hawakuwa na nafasi sana katika bendi za muziki wa dansi, maarufu muziki wa rhumba.

Bendi zilikuwa zikifanya maonyesho kwa malengo ya kuwafanya wapenzi wa muziki wacheze. Bendi nyingine zilikuwa na taratibu za kutoa taarifa za wimbo ambao ulikuwa upigwe, jambo ambalo kwa sasa limebakia katika baadhi ya vikundi vya taarabu, katika utambulisho huo bendi ilitangaza jina la wimbo na staili ambayo wimbo huo utapigwa.

Hivyo mtangazaji wa bendi aliwataarifu wapenzi wa muziki kuwa wimbo unaofuata ni Rhumba au Chacha au Borelo au Charanga na kadhalika. Iliitegemewa wachezaji kucheza staili iliyotajwa, kila kitu kilifuata taratibu. Bendi nyingine pia zilikuwa na taratibu zilizotoa hata maelekezo ya aina ya nguo za kuvaa. Unadhifu ulikuwa muhimu. Kwa waliokuwa waingiaji wa muziki katika kumbi kama Bandari Grill wa New Africa na Simba Grill wa Kilimanjaro watakumbuka kulikuwa na mtu mlangoni aliyekuwa na tai nyingi, ukifika mlangoni na shati bila tai unaazimwa tai na baada ya kuivaa ndio unaruhusiwa kuingia ukumbini. Haya turudi kwa madansa, katika miaka ya 1960 bendi zilikuwa za vijana ambazo hazikupiga muziki wa rhumba zilikuwa na madansa wao, waliokuwa wakijiita majina kama Makumba Show, Tammi Show na kadhalika.

Tammi show, iliyoongozwa na Adam Kingui, msanii mwenye hadithi ndefu sana katika sanaa. Walikuwa wakicheza huku wakipigiwa muziki na bendi ya Flaming Stars ya akina Raphael Sabuni na Mohamed Mdoe mbele ya Forodhani Hotel. Hoteli hii ilikuwa kijiwe maarufu cha wapenda starehe Dar es salaam, kwa sasa ni jengo la Mahakama ya Rufaa. Mmoja wa madansa katika picha hii, wakati huo akijulikana kama Jifast, kwa sasa ni mpiga drums mkongwe katika moja ya bendi kubwa hapa nchini.

Ujio wa Luambo Luanzo Makiadi na bendi yake ya TP OK Jazz mwaka 1973, akiwa amesindikizana na kundi la madansa, uliamsha utamaduni wa kuwa na madansa katika bendi za rhumba. Utamaduni ambao umedumu mpaka leo.

Kama nilivyosema awali kumekuwa na safari ndefu katika fani ya madansa wa bendi za muziki wa rhumba. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, Umoja wa Vijana Dar es Salaam ulifikia hatua ya kupiga marufuku kazi hii. Katika tamko hilo pia ilitangazwa kupiga marufuku majina ya sifa ya wasanii kama Power Savimbi aliyekuwa akionyesha michezo ya nguvu kama kuvuta magari kwa nywele zake, pia kwa tamko hili ilipigwa marufuku shule za Chekechekea kuitwa za vidudu ingawa marufuku ya ‘Stage Show’ haikudumu sana, bendi ziliendelea na utaratibu huu uliowapa umaarufu madansa wengi wa wakati huo. Majina kama Abdallah Pangapanga, Chileshi Ally, Nkulu Wabangoi, Frida, Flora Homa ya Jiji, Ajelike Wakubenga, Eliza Kimondo na kadhalika yalikuwa maarufu katika anga za wapenzi wa muziki dansi.

Mmoja wa madansa wakongwe ni Tabu Mambosasa, ambaye kwa sasa ni mwanamuziki mwimbaji, alianza kuonekana baada ya kushinda mashindano ya kucheza dansi watoto, yaliyoendeshwa na bendi ya Orchestra Makassy pale ukumbi wa Amana, Ilala, mwaka 1988. Akapata ujasiri wa kujiunga na bendi ya International Africa Show iliyokuwa ikiongozwa na Kwempa Risasi, kisha akajiunga na kundi la Makutano Dancing Troupe moja ya makundi yaliyojiita Dancing Troupe, kisha akahamia DDC Kibisa. Kaka yake ambaye alikuwa kipa maarufu enzi hizo Athumani Mambosasa, alikuwa mpenzi wa bendi ya MK Group, akamshawishi kujiunga na kundi hilo. Ilipoanzishwa Washirika Tanzania Stars, Tabu akawa mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo maarufu. Baadaye akapitia MCA Band na baadaye Bantu Group.

Dansa mwingine ambaye kwa sasa yuko Mwanza akiendelea na kazi hiyo aliyoianza mwaka 2000 ni Nasra, ni ndugu na wanamuziki marehemu, mpiga drums Abbu Semhando na mpiga bezi Baker Semhando. Yeye alianza kucheza dansi mwaka 2000, bendi yake ya kwanza ilikuwa Mwenge Jazz, safari yake katika kazi hiyo ikampitisha Vijana Jazz, Fax Jazz Band, Mviko, Double M Sound, Extra Bongo, Bambino Sound, Mchinga Sound, TOT na Akudo Sound, akiwa na wenziye wa enzi zake akina Halima White, Queen Happy, Diana Aston Villa, waliokuwa maarufu enzi zao.

Wacheza shoo wakongwe wanakubali kuwa mambo mengi ni tofauti, zamani malipo yalikuwa ni posho baada ya kila onyesho au mshahara wa mwezi, siku hizi ni posho tu ambayo ukiangalia mara nyingine thamani yake ni ndogo kuliko waliyoipata zamani.

Na badiliko kubwa ni muda wa kucheza shoo, zamani ilikuwa muda mfupi usiozidi nusu saa kila dansi, muda uliobaki waliachiwa wapenzi waserebuke, siku hizi muda mwingi zaidi unatumika kwa madansa kucheza na wapenzi kulazimishwa kuwa waangaliaji tu.

Bendi nyingine zilikwepa kuwa na wacheza shoo wasichana kuondoa matatizo yaliyokuwa yakizikumba bendi hizo kutokana na mahusiano ya kimapenzi kati ya wana bendi, wivu na ugomvi yakawa yanapunguza ufanisi wa kazi.

Hivi karibuni kuna habari kwamba wacheza shoo wa bendi moja maarufu wamefukuzwa bendi baada ya kugombana na dansa mwenzao ambaye inadaiwa ni mpenzi wa kiongozi wa bendi hiyo.